Mgunda: Kundi gumu ila poa tu

KOCHA MKuu wa Simba, Juma Mgunda leo, Desemba 13 amesema kundi walilopangwa kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ni gumu lakini mbali na maandalizi watakayo fanya pia watatumia uzoefu waliokuwa nao kufuzu robo fainali.

Akizungumza na SpotiLeo, kocha huyo ameeleza ugumu wa kundi lao unatokana na timu zote walizopangwa nazo kushiriki kwenye kundi hilo la C zimekuwa zikishiriki mara kwa mara michuano hiyo kama ilivyo wao hivyo kitu cha muhimu ni kujipanga kuhakikisha wanatumia vizuri faida ya kushiriki mara kwa mara mashindano hayo.

“Tumepangwa kundi C na timu za Horoya AC,Raja CA na Vipers timu zote ni nzuri na tuna ziheshimu sababu ukiangalia rekodi zao mpaka zimefika hapo zimezitoa timu kubwa Afrika pengine kuliko sisi lakini hatuwezi kuziogopa hata sisi tupo hapo kwa uwezo wetu na wao wanalijua hilo tutapambana kuhakikisha tunatumia uzoefu wetu kusonga mbele hatua zinazo fuata,” amesema Mgunda.

Advertisement

Kocha huyo amesema kitu kizuri kwao wanataraji kukiongezea nguvu kikosi chao katika dirisha dogo usajili ambao anaamini utakuwa na faida kubwa katika hatua hiyo ya makundi.

Kocha huyo amesema nalengo yake ni kuwa kocha atakayeivusha timu hiyo kutoka robo fainali ilipokuwa ikiishia katika misimu mitatu mfululizo na kufika nusu fainali na hilo linawezekana kutokana na utayari waliokuwa nao.