DSM; “Alikufa mara nyingi!” Bila shaka unaweza ukajiuliza ina maana gani kauli hiyo? Ni nini? Nani? Ilikuwaje? Kwa nini?
Hilo ni onesho la kimuziki, utambaji hadithi na ushairi likiongozwa na msanii nguli nchini Mgunga Mwamnyenyelwa, likiwa ni onesho la hisani.
Mgunga ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika lisilo la kiserikali la Babawatoto, anasema maandalizi kuhusu onesho hilo ambalo yeye ndiye muongozaji mkuu yamekamilika na litafanyika Nyumba ya Utamaduni na Makumbusho ya Taifa, Dar es Salaam.
“Kila mtu anaweza kujiuliza alikufa mara nyingi maana yake nini, naomba wote tujumuike katika onesho letu la hisani ambalo limeandaliwa na Baba Watoto Organization na tutapata majibu;
“Onesho letu la kwanza litakuwa Septemba 28, 2023, la pili litafanyika Septemba 29,2023 na la tatu litafanyika Septemba 30,2023 eneo ni hilo hilo la Nyumba ya Utamaduni na Makumbusho ya Taifa.
“Septemba 28 na 29 tutaanza saa moja usiku kwa kiingilio cha Sh 50,000 mtu mmoja, isipokuwa Septemba 30 tutaanza saa nane mchana, ambapo wanafunzi kiingilio kitakuwa Sh 5,000,” amesema Mgunga aliyejijengea jina kubwa katika sanaa hiyo.
Mgunga alijijengea jina mwishoni mwa miaka ya 1990 hasa katika wimbo wa Tangulia Mwalimu uliokuwa mahususi kwa maombolezo ya msiba wa Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere aliyefariki dunia Oktoba 14, 1999, ambapo ubunifu wake ulikuwa kivutio kikubwa.
Pia miongoni mwa maonesho makubwa aliyotunga ama kuandaa ni kama vile Samaki wa Dhahabu, Wimbo wa Nyonga, Mfalme Saltan na Mwanae Guidon, Bongo Dar es Salaam, Mkwezi na Mnazi, Wimbo wa Jando na Sauti Kutoka Mazimbu.