Mhando achaguliwa mwenyekiti mpya TASWA
UCHAGUZI Mkuu wa Chama Cha Wandishi wa Habari za Michezo nchini (TASWA), umefanyika leo na kushuhudia Amir Mhando akichaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa Chama hicho.
WAJUMBE wa Chama cha Wandishi wa Habari za Michezo nchini (TASWA) wamemchagua Amiri Mhando kuwa mwenyekiti wao mpya.
Anachukua nafasi ya Juma Pinto ambaye muda wake madarakani umemalizika.
Mhando ameingia madarakani baada ya kupata kura 57 na kumshinda mpinzani wake Mbwana Shomari aliyepata kura 10 peke.
“Nawashukuru kwa imani mliyonipa na mimi ninawaahidi kuwatumikia na kuifikisha mbali Taswa, ikiwemo kuendesha semina mbalimbali za kuwajengea uwezo wandishi wote,” amesema Mhando huku akiomba ushirikiano kutoka Kwa wajumbe hao.
Katika uchaguzi huo uliofanyika jijini Dar es Salaam leo, Jumapili, nafasi ya Katibu Mkuu imechukuliwa na Alfred Lucas aliyepata kura 57 huku mpinzani wake Issa Ndokeji akipata kura tisa.
Imani Makongoro aliibuka mshindi katika nafasi ya Katibu Mkuu msaidizi baada ya kupata kura zote za ndio 68 .
Nafasi ya mweka hazina ilichukuliwa na Dina Ismail aliyepata kura za ndio 65 na walioshinda nafasi za wajumbe ni Timzo Kalugira aliyepata kura 62 na Nasyongelya Kilinga ambaye alipata kura 60.
Uchaguzi huo ambao ulisimamiwa na Baraza la Michezo nchini BMT, umefanyika kwa mara ya kwanza baada ya miaka kadhaa kupita bila kufanyika.