Mhasibu atekwa, achomwa moto kwa petroli

Prado lagonga lori, mfanyabiashara afa

JESHI la Polisi mkoani Pwani limesema mhasibu wa benki ya BOA tawi la Kahama ameuawa kwa kumwagiwa petroli na kuchomwa moto.

Inadaiwa kwamba mhasibu huyo alikuwa  amefika Kibaha kwa wazazi wake.

Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Pius Lutumo amemtaja marehemu ni Martha Towo (30) mkazi wa Kwa Mbonde wilayani Kibaha.

Advertisement

Kamanda Lutumo aliwaeleza waandishi wa habari mjini Kibaha jana kuwa chanzo cha mauaji hakijafahamika na wanaendelea kuchunguza.

Inadaiwa kuwa Martha alitekwa jioni ya Machi 3 mwaka huu na saa 4:30 usiku siku hiyo hiyo alikutwa akiungua katika maeneo ya Mitamba Kata ya Pangani.

“Watu wasiojulikana walimteka kisha kummwagia mafuta na kumchoma moto,” alisema.

Kamanda Lutumo alisema taarifa zilitolewa na wasamaria polisi wakafika eneo la tukio na kumchukua kisha kumpeleka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani ya Tumbi.

“Mgonjwa alihamishiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa uangalizi zaidi wa kimatibabu lakini alifariki Alhamisi Machi 9,” alisema.

Lutumo alisema kutokana na utata kuhusu tukio hilo, polisi wanaendelea kuchunguza chanzo cha Martha kutekwa na kuchomwa moto hadi akapoteza maisha.

/* */