Mhasibu Dar adaiwa kughushi bil 8.9/-

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imempandisha kizimbani mhasibu wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Alinanuswe Mwasasumbe na kumsomea mashtaka 13 ikiwemo moja la matumizi mabaya ya madaraka, 10 ya kughushi, moja la kutakatisha fedha haramu na kuisababishia halmashauri hasara ya zaidi ya Sh bilioni 8.9.

Mshtakiwa huyo alisomewa mashtaka mahakamani hapo jana na Wakili wa Serikali kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Fatuma Waziri mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Ferdnand Kihwonde.

Katika mashtaka ya matumizi mabaya ya madaraka inadaiwa kuwa kati ya Julai 1, 2019 na Juni 30, 2021, katika Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam, Mwasasumbe akiwa ni mtumishi wa umma alitumia madaraka yake vibaya kwa kushindwa kuingiza fedha za makusanyo ya mapato alizopaswa kuziingiza katika benki za NMB, CRDB, NBC na DCB.

Inadaiwa kwa kutenda kosa hilo alijinufaisha na kujipatia Sh 8,931,598,500 mali ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Katika mashtaka ya kughushi, Mwasasumbe anadaiwa kutengeneza nyaraka za uongo ambazo ni barua zenye kichwa kinachosema ‘kurudishwa fedha zilizotumika’ ikionesha fedha hizo zilirudishwa kama ilivyoagizwa na mamlaka kwa matumizi ya vibarua wa soko na matumizi mengine.

Barua hizo ziliandikwa kwa tarehe tofauti kati ya Julai 1, 2019 na Juni 30, 2021 vikiwa na kichwa taja hapo juu kwa mujibu wa mwezi husika, na zilikuwa na viwango tofauti vya fedha vilivyosababisha jumla hiyo ya Sh 8,941,598,500.

Katika shtaka la kutakatisha fedha haramu inadaiwa kati ya Julai 1, 2019 na Juni 30, 2021, Mwasasumbe alijipatia jumla ya Sh 8,913,598,500 huku akijua ni zao la makosa tangulizi ya matumizi mabaya ya madaraka na kughushi.

Katika shtaka la mwisho, inadaiwa kati ya Julai 1, 2019 na Juni 30, 2021, Mwasasumbe katika Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam, Mwasasumbe aliisababishia Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam hasara ya kiasi tajwa hapo juu. Upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi haujakamilika na kesi hiyo iliahirishwa hadi Julai 10, 2023.

Habari Zifananazo

Back to top button