Abuni teknolojia kudhibiti magari kugonga treni

TABORA; MHITIMU wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Alvine Antony amebuni teknolojia itakayozuia ajali kati ya treni na vyombo vya moto, ambazo zimekuwa zikitokea katika makutano ya njia za reli na barabara.

Akizungumza na waandishi wa habari jana wakati akielezea mfumo huo katika maonesho ya usalama wa reli ambayo yanafanyika kitaifa mkoani Tabora, alisema mfumo huo umeundwa ukiwa na uwezo wa kutambua treni inapokaribia makutano ya barabara na reli.

Teknolojia hiyo inawezesha taa za barabarani kuwaka kuzuia magari na mageti yanafunga pande zote kuruhusu treni kupita na baadaye milango hiyo kufunguka ili kuruhusu vyombo vya moto kupita na watembea kwa miguu.

Alvine alisema amefanya ubunifu huo kwa muda wa mwezi mmoja wakati wa masomo yake katika chuo hicho.

Aliomba serikali na wadau wa usafiri wa reli kumshika mkono kuboresha ubunifu huo ili kupunguza ajali katika makutano ya reli na barabara.

Alisema teknolojia hiyo inaweza kutumika kusaidia kuondokana na wimbi la ajali ambazo zimekuwa zikitokea katika makutano ya njia za reli na barabara nchini.

Ofisa Uhusiano wa NIT, Juma Manday alisema teknolojia hiyo itakuwa mwarobaini wa kupunguza ajali kwenye makutano hayo.

Alisema maeneo hayo yamekuwa yakikumbwa na matukio ya ajali za mara kwa mara lakini teknolojia hiyo kutoka NIT itasaidia kwa asilimia kubwa kupunguza ajali hizo.

 

Habari Zifananazo

Back to top button