Miaka 30 tangu afariki, Maneti bado ‘anaishi’

LEO Mei 31, 2024, ikiwa imetimia miaka 34 tangu alipofariki gwiji wa muziki Tanzania na mwimbaji mashuhuri Hemed Maneti Ulaya bado maudhui ya nyimbo zake  yana ujumbe kwa jamii.

Nyimbo kama Wifi zangu mna mambo, Mary Maria, Niliruka Ukuta,  Chiku, Bujumbura, Tambiko la Pambamoto (wimbo wa lugha ya kifipa), Penzi haligawanyiki na nyinginezo nyingi ni baadhi ya nyimbo ambazo zinaposikika masikioni mwa wengi zinaleta hisia ya mkongwe huyo, aliyeondoka angali bado anapendwa na wapenzi wa muziki nchini.

Ilikuwa jioni ya Mei 31, 1990 muda ambao masikio ya wapenzi wa michezo nchini yalisikia taarifa ya ukakasi iliyotangazwa na  Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD) katika kipindi cha michezo. Taarifa ile  ilizua taharuki kwa baadhi ya mashabiki na wapenzi wa muziki nchini.

Mara RTD inasikika kutoka kwa mtangazaji alipoutangazia umma kuwa mwanamuziki Hemed Maneti ‘Chiriku’ amefariki na kuanza kupiga wimbo wa Mary Maria.

   Hemed Maneti Ulaya ni nani?

Ingawa ni miaka mingi imepita lakini nyimbo zake zimekuwa zikipigwa na vyombo vya habari nchini hasa RTD, kuonesha jinsi gani alivyokuwa na kipaji cha aina yake  na uwezo mkubwa wa kutunga na kuimba.

Maneti alizaliwa kijijii cha Mamboleo Wilaya ya Muheza Mkoa wa Tanga mwaka 1954 na kufariki akiwa na miaka 36 tu.

Manlikuwa kiongozi na mwimbaji na alijiunga na bend ya vijana 1975 akitokea Cuban Marimba, amabpo alivuma na wimbo Ni Shauri ya Malezi Mabaya.

Kufariki kwa Maneti kumeacha pengo Vijana Jazz, kwani Vijana ya leo si ile ya miaka ya 1980 au 1990. Maneti alikuwa kiongozi, mwalimu, mlezi , mchapakazi  na mtu aliyethamini kazi yake na kulitumikia taifa lake kwa nguvu zote.

Alikuwa ni mvumilivu na wala hakubweteka na umaarufu kwa muda wote aliokuwa nao Vijana Jazz. Licha ya kuja na kupwa Maneit hakushawishika hata mara moja kuihama Vijana Jazz pamoja na kufuatwa na  bendi kadhaa za hapa nchini zikimtaka ahamie kwao.

Kuna msururu mrefu wa sifa na mchango mkubwa alioutoa marehemu Maneti katika mambo mbalimbali kupitia sanaa ya muziki.

Maneti alizikwa kijijini kwake baada ya umati mkubwa wa mashabiki na viongozi mbalimbali wa Chama cha Mapinduzi kutoa heshima zao za mwisho, huku wanamuziki wa Vijana Jazz wakiomboleza kwa mwezi mzima.

Bendi ya Vijana Jazz ilibaki Tanga mwezi wote wa Juni baada ya maziko yake kufanyika Juni 3, 1990.

Kipaji cha utunzi na uimbaji alichojaliwa gwiji huyu  kilionekana wazi katika tungo zake maridhawa.

Vijana ilimilikiwa na Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM),  ambapo mwaka 1985 Maneti alitunga wimbo wa kampeni kwa ajili ya mgombea pekee wa urais wa Tanzania wakati huo, Ali Hassan Mwinyi. Wanaokumbuka kuna sehemu anasema Ali Hassan Mwinyi apewe kura za ndiyo..

Mwanamuziki huyo alikuwa mwanasiasa safi ambaye hakuhutubia kwenye mikutano ya siasa, bali aliuonesha uanasiasa wake kupitia jukwaa la muziki.

Hakuwa nyuma katika masuala ya ukombozi na kutetea amani, rejea wimbo wa Magaidi wa Msumbiji aliutunga mwaka 1987. Wimbo huu pia ulitokea kuwa kipenzi cha watu na ni moja kati ya kazi za kukumbukwa.

Nyimbo nyingine za siasa ni Operesheni Maduka, Vijana Nguzo na Jeuri ya Chama, Muungano Umekamilika,Tamasha la Vijana Moshi, Rushwa Adui wa Haki, Mwenge Umulike Nje ya Mipaka ya Tanzania na nyingine nyingi.

Mbali na nyimbo za siasa Maneti alionesha kipaji chake pia katika tungo za mapenzi, kiasi kwamba tungo zake nyingi bado vinawakosha wengi hadi leo.

Zipo baadhi alizotunga mwenyewe na nyingine zilitungwa na watu wengine lakini yeye akiwa mwimbaji.

Baadhi ya nyimbo hizo za mapenzi ni Mary Maria, Penzi haligawanyiki I na II, Chiku Saizi Yangu, Niliruka Ukuta (sehemu ya I na II mwaka 1975), Kosa la Wazazi, Maggy Wanipa Mateso, Ilikuwa Lifti tu, Aza, Pili Wangu Nihurumie , Penzi Halina Umaarufu, Heshima ya Mtu na Chaurembo.

Pia zipo Wifi Zangu,  Matata Matata, Mudinde, Masimango, Vituko vya Ambhi, Masido,  Nsabi,  Watoto wanalia sana, Amba Kawa baharia, Wajue wana Koka, Jirekebishe, Safari yetu Mbeya na Bujumbura.

Alipojiunga na Vijana Jazz Maneti alipewa uongozi msaidizi wa bendi hadi mwaka 1982 alipoteuliwa kuwa kiongozi wa bendi.

Bendi ya Vijana chini yake ilipitia mitindo mbalimbali ikiwemo Koka Koka, Takatuka, Hekaheka, Pamba Moto I na II na Pamba Moto Shambulia na hapo ndipo alipachikwa majina mengi mojawapo ni Chiriku na Simba Mwendapole. Chiriku lilimkaa mpaka likaonekana kama moja ya majina yake halisi.

  Wananchi wanamzungumziaje?

Kapteni Mstaafu,  Alex Kapama  anasema bendi hiyo ilipitia misukosuko mingi ikiwemo ya kuhama kwa wanamuziki nyota, lakini kutokana na uongozi wake imara, gwiji huo aliweza kuisimamia bendi vizuri bila kuyumba.

Anawataja baadhi ya wanamuziki hao ambao kwa nyakati tofauti walihama ni Cosmas Chidumule, Adam Bakari ‘Sauti ya Zege’, Jerry Nashoni ‘Dudumizi’, Mohammed Gotagota, Komandoo Hamza Kalala ambaye aliondoka na baadaye kurejea tena kabla ya kuihama tena na kwenda Washirika Tanzania Stars ‘Watunjatanjata’ pamoja na Eddy Sheggy.

Wengine ni Hassan Dalali, Athumani Momba, Msafiri Haroub ambao nao, kama Kalala, waliihama bendi hiyo na kurejea tena, Kida Waziri na Mohammed Shaweji.

Naye Shabiki wa Maneti,  Stephen Minja anasema kutokana na kazi nzuri aliyoifanyia CCM wanapaswa kumuenzi ikiwa ni pamoja na kuhakikisha Vijana Jazz inafanya vizuri kwa kupata ufadhili na usimamizi mzuri.

Anasema bado anamkumbuka gwiji huyo kwa weledi wake wa kutunga nyimbo na sauti na uwezo wake wa kuchanganya sauti.

“Nikiri kwamba pengo la Maneti bado halijazibika kutokana na kuwa Vijana Jazz haiko imara kama alivyokuwa anaisimamia Chiriku,” anasema.

Minja anatoa rai kwa UVCCM kumuenzi Maneti kwa kuipa heshima kama bendi ya chama.

“Mimi kila ninaposikia ule wimbo wake wa Mary Maria nakumbuka tangazo la kifo chake, ambao RTD walitumia baadhi ya mistari kurudia rudia tangazo la kifo,” anasema Minja..

Anasema Maneti alifanyakazi kubwa iliyoacha alama hadi leo, UVCCM walimteua Said Hamis ‘msukosuko’ kuendeleza na kuigiza sauti ya Maneti.

Anasema kipaji chake kilianza kuonekana tangu akiwa shule ya msingi na alifanya kazi kwenye bendi ya Vijana Jazz kwa miaka 17

Habari Zifananazo

Back to top button