WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Moringe Sokoine leo anatimiza miaka 39 tangu kufariki dunia Aprili 12, 1984.
Sokoine alikufa katika ajali ya gari eneo la Wami-Dakawa, Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro akiwa njiani kurejea Dar es Salaam akitokea mjini Dodoma alikokuwa akishiriki vikao vya Bunge.
Aliwahi kuwa Waziri Mkuu mara mbili, mwaka 1977 hadi Novemba 7, 1980, Februari 1983 hadi kifo chake.
Uongozi wake ulionekana kuwa wa mfano kwa jinsi alivyokuwa na uadilifu na kufuatilia utendaji kazi huku akikemea ulaji rushwa na ubadhirifu wa mali za umma enzi za uhai wake.
Alikuwa ni kiongozi anayeamini katika haki, ukweli na hakupenda uzembe na alikemea vitendo mbalimbali viovu.
Miongoni mwa hotuba zake ni ile ya uwajibikaji na wajibu wa viongozi aliyotoa Machi 26, 1983 wakati akifunga semina ya viongozi wa serikali na mashirika ya umma.
Alisema: “Serikali iko tayari kuwalinda watumishi wa serikali wanaoheshimu taratibu na miiko ya kazi. Ni muhimu tutafute ukweli wa kuondosha dosari zote.”

HADITHI ZA KUSHINDWA
Sokoine alichoka kusikia hadithi za kushindwa baada ya kusema kuwa wananchi wamechoshwa kusikia hadithi za kushindwa kila siku na kuwataka viongozi watakaoshindwa kuleta ufanisi katika maeneo ya usimamizi wao au wapunguziwe madaraka kama si kuondolewa kabisa.
“Umma unatutegemea kushinda na si tushindwe. Viongozi wa serikali na mashirika lengo na shabaha yetu ni kupata ushindi katika matatizo yetu,” alisema.
USALAMA
Alisema wajibu wa kihistoria wa serikali ni kuhakikisha usalama na amani nchini kwani wananchi wanategemea serikali yao italinda maisha yao na mali zao na huo ni wajibu wa msingi kabisa wa serikali.
WAHUJUMU
“Ole wao wale wanaotumia nafasi zao za umma na serikali, kuiba, kuhujumu uchumi, kupokea rushwa maana salama yao ni kudra za Mwenyezi Mungu labda nisiwajue.”
Hayo ni maneno aliyowahi kuyatamka Sokoine na mzalendo wa taifa hili wakati akihutubia kwenye mkutano wa Kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) mjini Dodoma wakati huo vita ya kupambana na suala la uzembe katika kazi, ulanguzi, rushwa na biashara ya magendo ukiwa umepamba moto.

ALIPENDA UJAMAA
Sokoine alikuwa hasa mzalendo na aliyependa siasa za ujamaa na hata kupelekea kumwomba Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ruhusa ya kusimama kwa muda kama waziri mkuu ili aende kusomea zaidi mambo ya ujamaa nchi za nje.
Ilikuwa mwaka 1981 na 1983 alirudi kuendelea kama Waziri Mkuu hadi mauti ilipomkuta.
RAIS SAMIA
Kama ambavyo kiongozi huyo alikuwa akipenda haki na kukemea uzembe ndivyo ambavyo hata Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akifanya na kuonesha kuchukizwa na uzembe kwa baadhi ya watendaji.
Kila anapokutana na watendaji mbalimbali amekuwa akisisitiza suala la uwajibikaji na huduma zitolewe kwa umma.
Mwaka juzi Rais Samia aliyataka mashirika yasiyokuwa ya kiserikali kuongeza uwazi na uwajibikaji katika kazi zao pamoja na kwenda sambamba na vipaumbele na mipango ya serikali ili yaweze kulea tija katika jamii.
Alisema hayo katika mkutano wa mwaka wa mashirika ya umma yasiyokuwa ya kiserikali uliofanyika Dodoma mwaka 2021.
Pia, Rais Samia ametatua changamoto mbalimbali kwa mfano za kisiasa namna alivyokutana na vyama vya upinzani kuleta suluhu, kuimarisha ushirikiano na kukemea vitendo vya kibadhirifu dhidi ya baadhi ya watumishi wa umma.
Hayo anayoyafanya kiongozi huyu yanaonesha namna gani serikali inaendelea kuenzi mazuri yaliyofanywa na viongozi wengine waliopita kwa lengo la kuleta maendeleo kwa wananchi wake.
Wakati watu wakikumbuka kifo cha Sokoine wanajivunia yeye kwa kile alichokifanya kwa kipindi kifupi kwa miaka hiyo na hatimaye wengine wakashika na kuendeleza pale alipoishia.
HISTORIA YAKE
Sokoine alizaliwa Agosti Mosi, 1938 katika Wilaya ya Maasai Land inayofahamika kwa sasa kama Wilaya ya Monduli, iliyoko mkoani Arusha.
Alipata elimu yake ya msingi Monduli, akafaulu kujiunga na Shule ya Sekondari Umbwe kuanzia mwaka 1948 mpaka 1958 alipomaliza hapo alijiunga rasmi na chama cha TANU mwaka 1961, kisha alipata nafasi ya kwenda nchini Ujerumani mwaka 1962 mpaka 1963 kusomea uongozi na utawala na aliporudi akateuliwa kuwa Ofisa Mtendaji Wilaya ya Maasai Land.

Kutokana na ufanyakazi wake uliotukuka wilayani Monduli, wananchi wakamchagua kuwa Mbunge wa Monduli na ufanisi wake kiutendaji ulionekana machoni mwa watendaji wakuu wa serikali na Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere na akachaguliwa kuwa Naibu wa Wizara ya Mawasiliano na Usafiri mwaka 1967.
Mwaka 1972 aliteuliwa kuwa Waziri wa Usalama na hatimaye mwaka 1977 aliteuliwa rasmi kuwa Waziri Mkuu.