MIAKA 39 KIFO CHA SOKOINE

Sokoine (Kulia) akiwa na Mwalimu Nyerere

LEO ni kumbukumbu ya miaka 39 ya kifo cha Waziri Mkuu wa Tanzania, Edward Moringe Sokoine, kilichotokea Aprili 12, 1984 kwa ajali ya gari eneo la Wami Dakawa mkoani Morogoro akitokea Dodoma kwenye kikao.

Tukio hilo lilileta simanzi na si tu kwa Watanzania bali kwa viongozi wengine waliofanya naye kazi na waliomfahamu utendaji wake kwa sababu alikuwa mtu wa haki, mpambanaji wa wala rushwa, aliwachukia wahujumu uchumi na maovu mengine katika jamii.

Advertisement

Sifa zake ndizo zikanifanya nimtafute Ofisa Mwandamizi wa Polisi mstaafu, Tatu Ntimizi (75), ambaye alimfahamu kwa kiasi kikubwa Sokoine kutokana na majukumu yake wakati huo na kuna nyakati Sokoine alimwita Tatu akiwa kazini na kwenda kumpongeza kwa kazi nzuri anayofanya ya kuendesha kesi za uhujumu uchumi na nyingine kubwa zenye maslahi ya taifa.

Nilimpigia simu mama Tatu Ntimizi na kuzungumza naye kisha akanipa miadi ya kuonana naye kesho yake kwa ajili ya mahojiano zaidi kuhusu alivyomfahamu Sokoine na bila kusita nikafunga safari mapema asubuhi kwenda katika moja ya makazi yake eneo la Misugusugu, Kibaha mkoani Pwani.

Tatu Ntimizi alikuwa mmoja wa watumishi wa serikali aliyefanya kazi katika Jeshi la Polisi na kuwa na vyeo tofauti, akafanya kazi mahakamani kama Mwendesha Mashitaka Kiongozi katika Mahakama ya Kivukoni, Kisutu (Dar es Salaam na Moshi mkoani Kilimanjaro.

Katika majukumu yake hayo aliyatekeleza kwa nidhamu, weledi na uadilifu na kupanda vyeo pamoja na kushika nyadhifa kama kaimu kamanda wa polisi, mkuu wa wilaya, mbunge na naibu waziri.

Akizungumzia siku ya ajali, mama Ntimizi anasema alikuwa akikaimu nafasi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani wakati ajali inatokea.

Tatu Ntimizi

“Nakumbuka siku ya ajali nilikuwa Kaimu Kamanda wa Polisi Pwani, hivyo tulitaarifiwa kuwa tuwepo kwenye mipaka ya mikoa kupokea msafara wa Waziri Mkuu Sokoine aliyekuwa akitoka Dodoma kuelekea Dar es Salaam, nikatoka na askari wangu kusubiri msafara,” anasema mama Ntimizi.

Anabainisha kwa kawaida katika msafara kama huo, kila Kamanda wa Polisi wa Mkoa ambako kiongozi atapita humpokea mpakani na kuongoza msafara hadi mpakani mwa mkoa mwingine mpaka kiongozi afike anakokwenda.

“RPC wa Dodoma akatutaarifu wa Morogoro na Pwani, alipoanza safari Dodoma, akatutaarifu na tukajipanga kwenye mipaka yetu mimi nikaenda pale Bwawani- mpakani mwa Morogoro na Pwani,” anasema mama Ntimizi.

Anabainisha kuwa taarifa alizopewa na RPC wa Morogoro ni kwamba afike hapo Bwawani mpakani saa tisa alasiri siku hiyo ya Aprili 12, 1984.

“Kila wakisogea kutoka Dodoma wanatoa taarifa na sisi tunajiandaa tukafika Bwawani, saa tisa ikafika nasubiri kwamba nitapigiwa simu, wapi saa tisa na nusu RPC-Morogoro ananipigia anasema, vipi!..uko mpakani? Nikamwambia ndio, akasema sisi tuko hospitali, Morogoro. Nikamwambia imekuaje, akasema unaongelea wapi, nikamwambia niko na askari akasema nenda pembeni, nikaenda akasema bahati mbaya Waziri Mkuu kapata ajali na gari la hao wapigania uhuru.”

Anaendelea kusimulia kuwa, baada ya taarifa hiyo, aliulizwa na RPC wa Morogoro kama anaweza kwenda Morogoro lakini alimjibu hawezi na wakati huo nguvu zikamuishia kwani alijisikia vibaya na kumwambia acha arudi.

“Niliishiwa nguvu, nikatoka pale Bwawani hata mwendo kumwambia askari nenda nilishindwa, tukarudi na nikiwa njiani nikamwambia Kamanda wangu wa Pwani yaliyotokea na kumtaarifu hali yangu si nzuri narudi Dar es Salaam nyumbani,” anabainisha mama Ntimizi.

Anasema siku mwili wa Sokoine unapelekwa katika Ukumbi wa Diamond Jubilee kuagwa alishiriki lakini akashindwa kumtazama kwa sababu alimzoea na kila akivuta picha anamkumbuka jinsi alivyokuwa akimuongoza katika misafara yake na kubwa zaidi ni wakati alipomwita ofisini kumpongeza kwa kufanya kazi kwa uadilifu.

“Nilishindwa kumtazama siku ya kumuaga pale Diamond Jubilee, nikawa navuta picha nakumbuka wakati naongoza msafara wake kumrudisha nyumbani baada ya kutoka kwenye majukumu, namwambia kamanda, tumeshakufikisha, sisi tunaondoka, anasema haya mama karibu nyumbani,” anasimulia mama Ntimizi kwa huzuni.

Anasema, akikumbuka hayo, anajisikia vibaya kwa sababu anamkumbuka Sokoine alikuwa kama baba yake, lakini pia kiongozi mkubwa mwenye busara na mpenda haki na alikuwa akifanya kazi karibu naye katika misafara ya kwenda Dodoma kikazi au mingine Dar es Salaam na zaidi ni siku aliyomuita ofisini kwake.

Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine mkoani Morogoro.

Akizungumzia jinsi Waziri Mkuu alivyomuita ofisini kwake kumpongeza kwa kazi nzuri aliyokuwa akifanya ya kuendesha kesi za uhaini kwa weledi na watuhumiwa kutiwa hatiani na kuhukumiwa, mama Ntimizi anasimulia.

“Mwaka 1974 nikiwa ndani ya Jeshi la Polisi nimeshafanya kazi kwa muda sasa nikateuliwa kufanya kazi mahakamani kama mwendesha mashitaka, nilifanya kazi mahakama ya Kivukoni, kisha nikaenda Mahakama ya Moshi na mwaka 1976 nikarudi Dar baada ya mume wangu ambaye naye alikuwa askari polisi kuhamishiwa Dar.

Anasema akapelekwa kuwa Mwendesha Mashitaka kiongozi katika Mahakama ya Kisutu na wakati huo kesi za uhujumu uchumi, mauaji, rushwa na nyingine kubwa zilikuwa zinavuma.

“Nakumbuka kesi za Kisutu nyingi zilikuwa ngumu kama za uhaini na mauaji na mimi ndiye niliyekuwa naziendesha, wakati mwingine unapata kesi ina mashitaka 100 na yote unatakiwa uyafanyie kazi,” anasema.

Anasimulia kuwa katika kuendesha kesi hizo, kesi iliyompa ugumu na kufikia hata kuhatarisha maisha yake ilikuwa ya uhaini yenye watuhumiwa 13 ya mwaka 1983 iliyowahusisha Zakaria Hans Pope na Anko Tom.

“Nilipata ugumu na vishawishi, ila nilivishinda na wakati huo nilipewa ulinzi nilikuwa nafanya kazi kipindi cha Mwendesha Mashitaka wa Serikali (DPP), Masaba na wakati huo Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) alikuwa Lemomo.

Anasema katika kesi hiyo, baada ya vitisho DCI akampa ulinzi hadi nyumbani na aliendelea kusimamia na kuongoza mashitaka kwa watuhumiwa kwa kutafuta vielelezo na ushahidi na mwisho watuhumiwa hao walihukumiwa wote kifungu cha maisha jela.

Hata hivyo, baadaye viongozi walioingia madarakani waliwaachia kwa huruma.

“Nilifanya kazi kwa moyo wangu kwa weledi kwa kuangalia maslahi ya taifa langu, habari zangu zikaenea za utendaji kazi na kusimamia kesi kubwa na nzito kama hizo, ndipo siku moja nikiendelea na kesi kwa Jaji Koroso nikaletewa ujumbe naitwa na Waziri Mkuu Sokoine,” anasema Ntimizi.

Anasimulia kuwa akiwa anaendelea na kesi, alifika RPC wa Dar es Salaam, Daudi David akamwambia anaitwa na Waziri Mkuu Sokoine ofisini kwake muda huo.

Anasema hata Jaji Koroso alishangaa, akamruhusu na wakati akitoka alimkuta RPC nje pamoja na DPP-Masaba na DCI-Lemomo na alijisemesha mwenyewe labda wanadhani kuna rushwa amekula, ila akaenda asijue alichoitiwa, tena chini ya viongozi wake.

Hayati Edward Sokoine

“Nikafika Ofisini kwa Waziri Mkuu Sokoine, akatukaribisha, karibu mama, karibu sana, He Lemomo huyu mama anafanya kazi mahakama ya wapi? Akajibu Kisutu, akasema nimesikia habari zake, kesi nyingi za uhujumu uchumi watuhumiwa wake wanapatikana na hatia na kuhukumiwa, je, ni kweli?

Anasema Masaba na Lemomo kwa pamoja wakajibu ni kweli na ndio sababu tulimpeleka pale awe kiongozi wa mahakama ile lakini pia ndiye msimamizi wa mahakama zote za Dar es Salaam.

Mama Ntimizi anasema, Sokoine kusikia hivyo akasimama akampongeza kwa kumshika mkono.

“Akaniambia hongera sana mama, asante mwanangu endelea na uaminifu wako, lakini Lemumu, mbona hamumpeleki Bukoba akeendeshe kesi ya Kugi’s? DPP akasema huyu anaendesha kesi za eneo la utawala wake, tukitaka kumpeleka huko inabidi hapa tufute mamlaka yake tumpe ya huku. Sokoine akasema hapana msimuondoe, akasema kwani Kugis hawezi kuletwa hapa (Dar es Salaam), DPP akasema hapana alitenda kosa akiwa Bukoba,” anasimulia mama Ntimizi.

Mama Ntimizi anaendelea kusema, Waziri Sokoine akamwambia DPP-Masaba, basi wasimuamishe mama Ntimizi, bali wamuache hapo hapo aendelee kufanya kazi hapo na kisha akawakaribisha chai, ambayo anasema alishindwa kunywa mbele za wakubwa wake.

“Niliogopa, ila akasema kunywa chai mama, basi nikanywa kikombe kimoja hata sikuweza kumaliza, tukamaliza tukaaga nikatoka kurudi kazini mahakamani, nilifurahi sana, nikamwambia Jaji Koroso niliitwa kupongezwa na Waziri Mkuu Sokoine akafurahi akasema endelea na kazi,” anasimulia mama Ntimizi.

Ntimizi anahitimisha kwa kusema Sokoine alikuwa kiongozi mpenda haki, mwenye uchungu na nchi yake na asiyependa kuona rasilimali za nchi zinatapanywa na wachache, bali alitaka kuona jamii na nchi vinaendelea na kuwa na taifa lenye haki, maadili na weledi katika kazi.

Anatumia nafasi hii kuwashauri watendaji wa serikali na wengine kila mmoja katika eneo lake kufanya kazi kwa bidii na kuacha wizi, uhujumu uchumi ambao ni sumu ya maendeleo katika taifa lolote.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *