MIAKA 60 YA MUUNGANO WA TANGANYIKA NA ZANZIBAR

INEC yawa kielelezo uchaguzi huru, wa kuaminika

TAIFA linapoadhimisha miaka 60 ya Muungano, Watanzania tunajivuna kuwa Tanzania imekuwa miongoni mwa nchi zenye taasisi imara na madhubuti ambazo taratibu zake za uanzishwaji na uendeshwaji zipo kikatiba na kisheria.

Taasisi hizi zinafanya kazi kama vidole vya mkono wa mwanadamu kwani vinasaidiana kuhakikisha nchi inakwenda vizuri katika nyanja zote za kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Baadhi ya taasisi ni changa na baadhi ni kongwe, lakini zote ni muhimu kwani hata zile changa pamoja na uchanga wao, zinatoa mchango mkubwa katika utekelezaji wa majukumu yake na kutoa mchango katika kusukuma gurudumu la maendeleo. Katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wapo viongozi wa kuchaguliwa katika ngazi mbalimbali.

Hawa ndio wanaotunga na kusimamia sheria, sera, mipango na mikakati ya kuwaletea maendeleo wananchi wanaowachagua ili kushika nafasi walizonazo.

Katika kuadhimisha miaka 60 ya Muungano na kuwazungumzia viongozi waliongoza taifa hili kwa mafanikio makubwa, ni vigumu kutoitaja Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) inayotimiza umri wa miaka 31 tangu ilipoanzishwa Januari 13, 1993 wakati huo ikijulikana kama Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Chombo hiki kimekuwa na miongo mitatu ya kuendesha chaguzi zenye weledi na zinazozingatia katiba, sheria, kanuni na miongozo mbalimbali inayotolewa na tume. Aidha, ni muhimu kukumbuka kwamba Tume hii ambayo ni taasisi ya Muungano, chimbuko lake ni utashi wa kisiasa. Februari 7, 1991 aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi aliteua Tume ya watu 40 iliyoongozwa na aliyekuwa Jaji Mkuu wa Tanzania, Francis Nyalali.

Tume hiyo iliyofahamika kwa jina maarufu la Tume ya Nyalali ilikusanya maoni ya wananchi kuhusu kuendelea au kutoendelea na mfumo wa chama kimoja cha siasa. Baada ya kukusanya maoni, asilimia 80 ya Watanzania walitaka kuwapo chama kimoja na asilimia 20 walitaka mfumo wa vyama vingi vya siasa.

Licha ya maoni ya wananchi wengi katika ripoti ya tume hiyo kupendekeza mfumo wa chama kimoja, serikali
iliona busara Tanzania kuingia katika mfumo wa vyama vingi ili kuimarisha demokrasia.

Aidha, ripoti ya tume ilipendekeza iundwe upya Tume itakayosimamia uchaguzi nchini chini ya mfumo wa vyama vingi vya siasa.

Mapendekezo hayo ndio yaliyowezesha kuundwa kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ambayo sasa inajulikana kama Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).

Kutokana na mapendekezo hayo, serikali ilifanya marekebisho ya Katiba na sheria mbalimbali za uchaguzi ili kuendana na mfumo wa vyama vingi. Sura ya 3 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, ilirekebishwa na kufanya Tanzania kuwa taifa linalofuata mfumo wa siasa wa vyama vingi.

Aidha, Sheria ya Vyama vya Siasa Namba 5 ya Mwaka 1992 ilirekebishwa kuruhusu mfumo wa vyama vingi vya siasa.

Sheria ya Taifa ya Uchaguzi Namba 1 ya Mwaka 1985, Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa Namba 4 ya Mwaka 1979 na sheria zinazoendana pia zilirekebishwa ili kuondokana na matakwa ya chama kimoja na kuruhusu mfumo wa vyama vingi.

Hivyo, mapendekezo ya Tume ya Jaji Nyalali yalisababisha kuundwa kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Januari 13, 1993 na Rais Mwinyi aliwateua wajumbe wa Tume Januari 14, 1993.

 

Tume iliundwa chini ya Ibara ya 74(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977. Ibara hiyo inaeleza namna wajumbe wa Tume watakavyopatikana na sifa wanazotakiwa kuwa nazo.

Aidha, Ibara ya 74(3) ya Katiba inaelezea watu ambao hawatakuwa na sifa ya kuteuliwa kuwa wajumbe wa tume. Kwa mujibu wa Ibara ya 74(6) na 78 za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, zikisomwa pamoja na Kifungu cha 10(1) cha Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Namba 2 ya Mwaka 2024, majukumu ya Tume ni pamoja na kusimamia na kuratibu uandikishaji wa wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa Rais na Wabunge katika Jamhuri ya Muungano na Madiwani kwa Tanzania Bara.

Mengine ni kusimamia na kuratibu uendeshaji wa uchaguzi wa Rais na Wabunge wa Jamhuri ya Muungano na Uchaguzi wa Madiwani kwa Tanzania Bara.

Majukumu mengine ni kuchunguza mipaka na kuigawa Jamhuri ya Muungano katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya uchaguzi wa Wabunge, kuteua na kuwatangaza wabunge wanawake wa viti maalumu katika Jamhuri ya Muungano na madiwani wanawake wa viti maalumu kwa Tanzania Bara, kuandaa na kusimamia kanuni za maadili ya uchaguzi pamoja na kutoa elimu ya mpiga kura nchini.

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Ramadhan Kailima.

Aidha, Tume inawajibika kuratibu na kusimamia taasisi na asasi zinazotoa elimu ya mpiga kura, kuratibu na kusajili waangalizi wa uchaguzi na kuajiri au kuteua watumishi na watendaji wa Tume kwa kadri itakavyohitajika.

Haya yanafanyika kwa kuzingatia masharti ya Sheria ya Utumishi wa Umma na masharti mengine yatakayowekwa na Tume na kutekeleza majukumu mengine yoyote kama yalivyoainishwa kwenye katiba au sheria nyingine yoyote.

Tume hii inafanya kazi zake kwa uhuru, uwazi na weledi mkubwa. Uhuru huo msingi wake ni katiba kwa kuwa Ibara ya 74(7) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Mwaka 1977 inatamka kwamba: “Kwa madhumuni ya utekelezaji bora wa majukumu yake yaliyoainishwa katika ibara hii, Tume ya Uchaguzi itakuwa ni idara huru inayojitegemea, itafanya maamuzi yake rasmi kuhusu utekelezaji wa majukumu yake kwa vikao….”.

Uhuru huo wa tume umesisitizwa zaidi kupitia Ibara ya 74(11) ya Katiba inayosema: “Katika kutekeleza madaraka yake kwa mujibu wa masharti ya katiba hii, Tume ya Uchaguzi haitalazimika kufuata amri au maagizo ya mtu yeyote au idara yoyote ya serikali, au maoni ya chama chochote cha siasa”.

Licha ya kutekeleza majukumu kwa mujibu wa katiba na sheria za uchaguzi, tume katika kuongeza weledi na uwazi katika utendaji wake ndani ya miaka 60 ya Muungano, imepanua wigo wa wadau inaowashirikisha katika hatua mbalimbali za utekelezaji wa majukumu ili kuweka uwazi na kuwapa wadau hao nafasi kutoa maoni yao. Wadau hao ni pamoja na vyama vya siasa, wapiga kura, vyombo vya habari, taasisi na asasi za kiraia, serikali, taasisi za dini, vyombo vya ulinzi na usalama, waangalizi wa uchaguzi, watu wenye ulemavu, wanawake, vijana na wazee.

Katika kuadhimisha miaka 60 ya Muungano kwa upande wa uchaguzi, Watanzania wanajivuna kuwa nchi yao imeshuhudia maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia yaliyoinufaisha Tume ya Taifa ya Uchaguzi na kuiwezesha kuvunja rekodi kwa kutangaza matokeo ya urais katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020 ndani ya saa 48.

Mafanikio hayo yametokana na matumizi ya mifumo ya uchaguzi ya kidijiti iliyosanifiwa na kujengwa na wataalamu wa ndani.

Matunda ya muungano pia yanaonekana katika ukuaji wa uchumi ulioiwezesha Tanzania kujitegemea kwa asilimia 100 katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020 kwa kugharamia shughuli zote za uchaguzi.

Hata sasa kuelekea maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa 2025, Tume inaendelea kufanya maandalizi yote bila kutegemea msaada wa wahisani.

Ushirikiano kati ya INEC na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) ni eneo lingine linaloonesha mafanikio ya miaka 60 ya Muungano. Msingi wa ushirikiano huo ni Ibara ya 74(13) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Mwaka 1977 na Kifungu cha 119(14) cha Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984 Toleo la 2010.

Ushirikiano wa tume hizi umewezesha kufanyika kwa chaguzi kuu, chaguzi za marudio na chaguzi ndogo kwa mafanikio katika kipindi hiki cha miaka 60 ya Muungano. Kwa kuwa wapiga kura wa Zanzibar ni sehemu ya wapiga kura wa Jamhuri ya Muungano, INEC na ZEC katika jitihada za kuwarahisishia wananchi kujiandikisha na kupiga kura kwa upande wa Zanzibar zimekubaliana kutumia vituo vya ZEC.

NEC ambayo sasa ni INEC katika kipindi hiki imefanikiwa kuwa na ofisi Zanzibar ili kuratibu shughuli zake. Tangu ianzishwe, Tume imesimamia na kuratibu Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani mara sita yaani mwaka 1995, 2000, 2005, 2010, 2015 na mwaka 2020. Aidha, tume iliratibu, kusimamia na kuendesha Uchaguzi wa Madiwani wa Mwaka 1994.

Habari Zifananazo

Back to top button