MIAKA MIWILI YA DK MWINYI : Mageuzi makubwa ukuaji sekta za fedha, biashara Zanzibar

RAIS wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi ametimiza miaka miwili ya kuwepo madarakani huku mwenyewe akijivunia mafanikio makubwa katika mageuzi ya sekta ya fedha, biashara na uchumi.

Dk Mwinyi akizungumza na wananchi Chake Chake, Pemba kuhusu miaka miwili ya uongozi wake alisema sekta hizo zimefanikiwa na kueleza kutakuwepo na mafanikio makubwa ya kiuchumi kutokana na watendaji aliowapa dhamana kuwa na ubunifu katika biashara.

Ndani ya miaka miwili ya uongozi wake, alisema mafanikio makubwa yamepatikana katika kujenga misingi mizuri ya demokrasia, utawala bora, mikakati ya kifedha na ukusanyaji mapato huku akiwapa majukumu watendaji katika sekta hiyo ambao wapo nje ya mfumo wa serikali yaani sekta binafsi.

“Nilipoingia madarakani nilikuwa na mikakati ya kuziimarisha sekta za fedha ikiwemo mabenki na mashirika ya bima kuona yanafanya shughuli zake na kwenda na kasi ya mageuzi yaliopo sasa na ndiyo maana nikawateua baadhi ya watendaji kutoka sekta binafsi kutoka nje ya Zanzibar kushika nafasi za uongozi,” alisema Dk Mwinyi.

Akizungumzia mafanikio ya miaka miwili ya Dk Mwinyi kwenye sekta ya kifedha na kibiashara, Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Bima Zanzibar (ZIC), Arafat Ali Haji, anasema moja ya maono ya Dk Mwinyi ni kuona taasisi za fedha za serikali zipo kwa ajili ya kufanya biashara na kuendeshwa katika mifumo ya kibiashara tofauti na ilivyozoeleka.

Haji anasema katika kutimiza ajenda yake hiyo, mashirika yote ya serikali amejaribu kuyabadilisha kwa kuweka wakuu wa taasisi hizo kutoka sekta binafsi za kibiashara ambapo katika kipindi kifupi matunda yameonekana.

Anasema lengo ni kuleta mabadiliko ya kiufanisi ambayo yanatokana na utendaji unaoendana na matakwa na mahitaji ya biashara ili mashirika hayo kuwa na tija na kuwa sehemu ya kuchangia pato la serikali.

Haji anasema wakati Dk Mwinyi anatimiza miaka miwili, ZIC ameliongezea ufanisi mkubwa kwa kulibadilisha kiutendaji kwa kushirikiana na wadau na kuondokana na utaratibu wa kufanya biashara wa kufikiria badala ya kuwatafuta wateja waliopo ili kutambua mahitaji yao.

Anasema hali hiyo inaongeza imani kwa wateja na kuliamini shirika hilo na kuongeza viwango vya biashara ambayo waliokuwa wakifanya na shirika hilo kwa ajili ya kwenda na kasi ya mabadiliko yanayotokana na sekta ya uwekezaji.

“Ndani ya mwaka mmoja shirika limeingia makubaliano na kampuni nyingi binafsi katika kukuza biashara, ikiwemo kumuwezesha mwananchi kununua bima yake kupitia simu ya mkononi,” anasema Haji.

Anasema lengo la kufanyakazi pamoja na taasisi za kibenki ni kuongeza mapato ya shirika hilo na kupunguza utegemezi wa kupata biashara kutoka sehemu moja.

Mkurugenzi huyo anasema kutokana na wingi wa wawekezaji wanaofika Zanzibar, shirika hilo limejipanga kutoa huduma kwa wawekezaji hao kwa sababu mwekezaji anahitaji kupata uhakika wa usalama wa mtaji wake.

“Uhakika huo ataupata endapo atawekeza katika majengo na kuyakatia bima na inapotokea ajali kufidiwa gharama zake bila ya kupata athari kubwa kwa sababu ikitokea mtaji wa mwekezaji umepotea hata Watanzania walioajiriwa wanaweza kukosa ajira na itakuwa na athari kwa ukuaji wa uchumi wa Zanzibar,” anasema Haji.

Aidha, alisema ndani ya miaka miwili ya Rais Mwinyi, sekta ya utalii imekua kwa kasi ambapo Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Amani Abeid Karume kwa mara ya kwanza kimekuwa na kiwango kikubwa cha uingiaji wageni.

Haji anasema shirika hilo limeanzisha bidhaa ambazo zitawapa unafuu watalii watapokuwa Zanzibar na wakikata bima ya afya au ya safari shirika hilo litamhakikishia atakapopata dharura yoyote iwe ya kiafya, msiba au kupoteza vitu vyake, shirika litalinda usalama wa mali zake.

Anaeleza hatua hiyo inawahakikishia watalii wanaofika Zanzibar kuwa salama hasa ikizingatiwa kuwa utalii ni sehemu kubwa ya ajira kwa Wazanzibari na Watanzania wote.

“Kasi ya idadi ya watalii wanaofika Zanzibar ni kubwa hivyo tumeanza kuwajengea uwezo watendaji wa shirika la bima ili kuwa na ubunifu wa kutambua ni bima gani kampuni za ndege zinahitaji ili kukidhi mahitaji ya ndege zinazofanya kazi za kusafirisha abiria na watalii,” anasema Haji.

Aidha, alisema kuwa kulingana na idadi ya Wazanzibari bado idadi ya ukataji wa bima ni ndogo na wengi wanakata bima kwa kutii sheria na sio kuona kuwa ni jambo la msingi katika maisha yao. Wana mikakati kufanya bima kuwa si ya hiari tena.

Aidha, alibainisha kwamba shirika hilo pia limefanikiwa na kutoa gawio kwa serikali na hivi karibuni wanatarajia kupeleka Sh bilioni moja kama sehemu ya kutoa faida kwa serikali.

Akizungumzia changamoto ya urasimu wa ulipaji wa fidia kwa wateja wa bima, Mkurugenzi huyo anasema utaratibu wa sasa umebadilika na sasa ndani ya siku 10 wateja wao wana uhakika wa kulipwa fidia baada ya kupata majanga na kulipwa kinachostahiki.

Anasema katika kulitekeleza hilo pia wanakumbana na changamoto ya madai hewa ambayo yanatengenezwa kwa lengo la kujipatia fedha ambapo katika mikakati yao wamejipanga kulivalia njuga tatizo hilo kwa kushirikiana na polisi.

Haji anasema wamejipanga na kujizatiti kutekeleza sera ya uchumi wa buluu kwa kuwafikia na kuwapatia huduma za bima wavuvi wote ikiwemo wale wanaojikita na kujiwekeza katika uvuvi wa bahari kuu.

Alisema hadi sasa bado wavuvi hawajazitumia kikamilifu huduma za bima.

Haji anaeleza kuwa changamoto zinazowakabili wavuvi ni kubwa wakati wakiwa katika shughuli zao ikiwemo ajali na wengine hupoteza maisha hivyo ukataji wa bima ni muhimu kunufaika na uchumi wa buluu.

“Tunatekeleza maagizo ya Rais wa Zanzibar, Dk Mwinyi ambaye anatimiza miaka miwili kuwepo madarakani akitutaka kuwafikia wajasiriamali mbalimbali ikiwemo wavuvi kuona wanakata bima ya vyombo vyao ili kuepukana na majanga yanayojitokeza baharini,” anasema Haji.

Anawataka Wazanzibari kuendelea kumuunga mkono Dk Mwinyi ili kumaliza kipindi chake cha kwanza cha uongozi akiwa ameviimarisha visiwa vya Zanzibar kiuchumi ikiwemo katika utekelezaji wa sera yake ya uwekezaji.

Anasema kuna matarajio makubwa ya mapato yanayotokana na bima kuongezeka kufuatia serikali kukodisha visiwa 10 kwa wawekezaji wakubwa duniani ambao wote hao watahitaji huduma za bima.

KAULI YA WAZIRI ANAYESIMAMIA FEDHA NA MIPANGO

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango, Dk Saada Mkuya, anasema mchango wa sekta ya fedha ikiwemo mabenki na taasisi za bima ni mkubwa katika ukuaji wa uchumi katika muelekeo wa mageuzi makubwa yanayotarajiwa kuwepo hivi sasa kufuatia kasi ya uwekezaji wa vitega uchumi.

Akitoa mfano, anasema ZIC imewekewa mikakati kuhakikisha inashiriki kikamilifu katika ukuaji wa uchumi pamoja na sekta ya uwekezaji wa viwanda katika sera ya uchumi wa buluu ikiwemo uwekezaji wa mafuta na gesi.

Anasema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imejipanga ikiwemo kuwajengea uwezo watendaji wa shirika hilo kuingia katika mageuzi makubwa ya uchumi hatua ambayo itajenga imani kwa wawekezaji katika uwekezaji wa miradi yao mikubwa.

“Hiyo ndiyo mikakati yetu ambapo tumewataka watendaji wa Shirika la Bima kujiweka tayari na mabadiliko yanayokuja ya ukuaji wa sekta ya fedha na biashara kuelekea uchumi wa buluu na kuchangia kikamilifu pato la taifa la uchumi,” anasema Dk Mkuya.

Akifafanua zaidi anasema katika kipindi cha miezi tisa kuanzia Julai 2021-2022, ZIC imekusanya Sh bilioni 21.20 sawa na asilimia 68 ya makisio ya kukusanya Sh bilioni 31.

Alimpongeza Dk Mwinyi kwani katika kipindi cha miaka miwili amefanya maboresho makubwa katika sekta za taasisi za fedha ikiwemo kuteua watendaji wanaokwenda na kasi ya mageuzi katika sekta binafsi.

“Hayo ndiyo mageuzi makubwa yaliyofanywa na Dk Mwinyi ambapo ameteua watendaji vijana ambao awali walikuwa katika sekta binafsi za fedha nje ya Zanzibar na kuwaleta nchini kuongoza na matunda yake tunayaona,” alisema Dk Mkuya.

Alizitaja baadhi ya taasisi za fedha zinazoshikiliwa na watendaji ambao walikuwa awali katika sekta binafsi kuwa ni pamoja na Benki ya Watu wa Zanzibar (BPZ) na Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB).

Habari Zifananazo

Back to top button