Michezo itumike kupunguza mimba na ndoa za utotoni -Mussai

WATOTO wa kike wametakiwa kujikita kwenye michezo hususani soka ili kuepuka mimba na ndoa za utotoni.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Mafunzo na Elimu ya Ufundi kutoka Wizara ya Elimu, Margarety Mussai akifunga mafunzo ya ukocha kwa mabinti kwa ngazi ya awali. ‘grassroot’.

Mafunzo hayo yameendeshwa na Shirika lisilo la Kiserikali la Karibu Tanzania Organization (KTO) chini ya usimamizi wa Shirikisho la Soka Tanzania  (TFF).

Margarety amesema, mabinti wa kike wakitumia muda mwingi kujishughulisha kwenye michezo hususani soka, kwanza watapata fursa ya kujiingizia kipato lakini pia itawasaidia kuepuka vishawishi vitakavyopelekea kupata mimba katika umri mdogo.

“Michezo inajenga ‘Confidence’   (kujiamini), na muda mwingi kwa sababu binti atatumia kwenye mazoezi basi itasaidia kuepuka vishawishi na  kupunguza  mimba na ndoa za utotoni. ” Amesisitiza

Katika kozi  hiyo, wasichana  13 wamehitimu mafunzo hayo ya awali ya  ukocha ‘Grassroot.

Kozi hiyo ya wiki mbili ililenga  kutoa elimu kwa washiriki namna  ya kukuza na kuendeleza vipaji vya kucheza mpira wa miguu kwa watoto wadogo kuanzia miaka minne hadi 12  katika ngazi ya awali.

Mkufunzi wa kozi hiyo  ya Grassroot  kutoka TFF,  Raymond Gweba amewapongeza washiriki wote waliojitokeza ili kukuza  mpira kwa vijana wenye umri mdogo lakini pia hakusita kusifia mwitikio mkubwa kwa washiriki katika kujifunza na kuuliza maswali.

“Walipoingia hapa ‘mentally’ zao zilijaa Usimba na Uyanga, baada ya kuwapiga msasa, sasa hivi ni makocha wa mpira sio wa Simba na Yanga…na kuna fomu maalum watajaza na kuingizwa kwenye data base (mfumo) wa TFF.   ” Amesema

Nae, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, Hawa Mniga akifunga mafunzo hayo, aliwataja wahitimu watumie vyema ujuzi waliopata kukuza soka la watoto hususani wa kike kuanzia ngazi za mitaa ili matunda yaonekane

Habari Zifananazo

Back to top button