Michezo ya kubahatisha yaendelea kunyooshewa vidole

MKUU mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Alex Malasusa  ameungwa mkono kuhusu kauli yake ya kuhimiza serikali ichukue hatua kuhusu michezo ya kubahatisha ili vijana wasibweteke.

Septemba 12 mwaka huu, Dk Alex Malasusa alipozungumza Dodoma wakati wa ibada ya ufunguzi wa mkutano wa tano wa wachungaji wote wa KKKT, aliomba serikali ichukue hatua kuhusu michezo ya bahati nasibu kwa kuwa inasababisha vijana wasifanye kazi.

Shehe wa Mkoa wa Mwanza, Hassan Kabeke, alisema viongozi wa dini wana wajibu wa kukemea kila jambo wanaloliona kuwa chukizo mbele za Mwenyezi Mungu.

Kabeke alisema Askofu Malasusa yuko sahihi kusema hilo kwa kuwa michezo ya kubahatisha ni kamali.

“Kwa kuwa michezo hii inafanyika hadharani, inawezekana sheria ya serikali imeruhusu, sisi kama viongozi wa dini wajibu wetu ni kuiomba tu serikali kulitazama jambo hili kwa sababu athari zake hazina afya kwa jamii yetu na kwa kizazi tunachokitengeneza,”alisema Shehe Kabeke

Aliongeza, “Kwa mfano leo tukiamka tukaona watoto wetu wamekuwa mashoga kwa mfano, maana yake tunawatengeneza watu wazima na wazee wajao kuwa mashoga, leo tukiamka tunakuta watoto wetu wamekuwa wavivu, hawafanyi kazi, hawafikirii kujiendeleza, hawafikirii kilimo, ufugaji, wanafikiria kubeti tu, kuna athari mbele yetu ambayo ni kubwa inayoweza kuliangamiza taifa.”

Askofu wa Kanisa la Anglikana, Jimbo la Newala, Oscar Mnung’a alisema michezo ya kubahatisha inasababisha vijana wengi kuwa  wazembe na hawafanyi kazi.

Mnung’a alisema michezo hiyo imesababisha watu wengine wawe na madeni kwa kuwa wanakopa fedha ili wacheze wakitarajia kupata fedha nyingi kwa wakati mmoja.

“Kama kiuchumi ni nzuri, kwa nini watu wanabeti mpira tu au mashindano ya magari na hawabeti nani ananunua zaidi maparachichi au mazao,” alihoji.

Profesa wa uchumi ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alisema kama fedha za michezo hiyo ya kamali zina muungano na masuala ya uzalishaji, haina tatizo.

Alitoa mfano kuwa ili mtu acheze  kamali, kuna vitu vingi ndani yake ikiwamo mashine zenyewe, nyumba zinazotumika kwa michezo hiyo vitu ambayo ni sehemu ya mchakato katika mnyororo wa uzalishaji, hivyo kwa mtazamo wa kiuchumi inaweza isiwe na shida japo kwa upande wa kidini inaweza kuwa tatizo.

“Ukiiangalia michezo hiyo, unaweza kuona ni sehemu ya uzalishaji kwa sababu wanaopata fedha wananunua vitu kama vile vocha na kuzifanya kampuni za simu kuendelea na kazi, wananunua vyakula na kusaidia wakulima kuendelea na uzalishaji, wafanyabiashara kuendelea na biashara lakini pia wakaenda kwa mama ntilie kununua vyakula,” alisema.

 

 

 

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x