Mifugo zaidi ya 400 yakamatwa, yauzwa Bonde la Ihefu –

MKUU wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera amesema wameuza mifugo zaidi ya 400 waliokamatwa kwenye eneo la ardhi oevu ya Bonde la Ihefu ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha wilayani Mbarali baada ya mahakama kutoa amri ya kutaifishwa kwa mifugo hiyo.

Amesema katika operesheni hiyo, wamekamata mifugo 6,000 na kukusanya faini ya zaidi ya Sh bilioni 620 kutokana na wafugaji hao kuingiza mifugo yao katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, hivyo kusababisha uharibifu mbalimbali.

Akizungumza kwa njia ya simu jana, Homera alisema kuwa katika hifadhi hiyo, wanyama na samaki wanakufa kutokana na ukame uliojitokeza na kwamba pamoja na kutoa maagizo mbalimbali wafugaji hawaelewi.

”Wenzetu (wafugaji) hawaelewi wanapoambiwa wasiingize mifugo yao kwenye vyanzo vya maji, wameendelea kupeleka mifugo yao wakati wa usiku kuanzia saa 3:00 na kuwatoa saa 10:00 alfajiri mradi tu waweze kuingia kwenye hifadhi,” alisema.

Aliongeza kuwa hawako tayari kuwa sehemu ya kuleta madhara na majanga kwenye nchi ikiwemo mkoa huo na kwamba watakuwa wakali kuhakikisha wanalinda vyanzo vya maji katika Bonde la Ihefu.

Katika operesheni hiyo wamefanikiwa kuondoa mifugo zaidi ya 200,000 katika eneo la Ihefu ambayo ilikuwa pembezoni mwa hifadhi na kueleza kuwa ushirikiano baina ya viongozi wa mkoa huo ulisaidia kuhakikisha mifugo inakwenda katika sehemu ambazo inastahili kukaa.

”Pia tulianza operesheni ya kuwaondoa wakulima ambao wako pembezoni mwa mto Ruaha wanaofanya shughuli za uvuvi, ufugaji wa samaki na kilimo kwani wamekuwa wakiziba mto ili kuvua samaki,” alieleza.

Alisema wamebaini uwepo wa matukio ya ujangili ambapo wamekamata meno ya tembo zaidi ya kilo 40 na juzi wamekamata meno ya tembo kilo 30, jambo linaloonesha kuna shughuli nyingi zilizokuwa zinafanyika katika Hifadhi ya Taifa ya Mto Ruaha ambazo hazikuwa zinatakiwa kwa mujibu wa sheria ya uhifadhi.

”Tayari tumeanza kuweka mpaka mkubwa kwa kutumia greda na kuweka bikoni zenye urefu wa meta mbili hadi meta moja na nusu ili kuhakikisha tunachonga barabara inayotenganisha Hifadhi ya Taifa Ruaha, makazi ya wananchi na mashamba yao,” alisema.

Alisisitiza kuwa licha ya kuwaondoa wakulima kwenye vyanzo vya maji maeneo ya Mbarali na kuzuia wale waliokuwa wanachepusha mto kuingia kwenye mashamba hasa wakati wa masika, maji yamekuwa yakipotea.

Homera alisema wameanza utekelezaji wa maagizo ya Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango ya kuwaondoa wananchi waishio milimali na katika hifadhi ili waondoke. Kamati za usalama zipo tayari kusimamia na kulinda vyanzo vya maji ili Rais (Samia Suluhu Hassan) anavyoiweka mipango yake ya kuleta maendeleo itimie kwa uhakika.

Septemba mwaka huu Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA), walianzisha oparesheni maalumu ya kuondoa zaidi ya mifugo 200,000 iliyovamia eneo la ardhi oevu ya Bonde la Ihefu ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha wilayani Mbarali.

Ilielezwa kuwa mifugo hiyo ilikuwa ikiingizwa na wafugaji kinyemela, hivyo kuhatarisha ikolojia ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha pamoja na Mto Ruaha Mkuu.

Aidha, walikuta mifugo zaidi ya 500 imekamatwa na askari wa Jeshi Usu ikiwa imehifadhiwa kwenye Kambi ya Ikoga Mpya ikidaiwa ilisagwa umbali wa zaidi ya kilometa 20 ndani ya hifadhi.

Homera alisema hali hiyo inahatarisha uwepo wa hifadhi hiyo ambayo ni miongoni mwa hifadhi kubwa pamoja na Mto Ruaha Mkuu ambao ni muhimu kwa maisha ya viumbe hai pamoja na miradi mikubwa ya umeme ukiwamo Mradi wa Bwawa la Julius Nyerere, Rufiji.

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x