Mifumo ya tiketi ifanye kazi – Mchengerwa
DAR ES SALAAM: WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mohamed Mchengerwa ameuelekeza Uongozi wa Wakala wa Mabasi ya Mwendokasi (DART) mifumo yote ya kieletroniki inafanya kazi.
Mchengerwa ameyasema hayo kwenye ziara yake kwa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) na kubaini mifumo ya kieletroniki ya DART ikiweo ya kukatisha tiketi haifanyi kazi na tiketi zinachanwa kwa mkono.
Kutokana na hali hiyo, Mchengerwa ameagiza wakala kuhakikisha mifumo ya Kieletroniki ambayo haifanyi kazi kuhakikisha inafanya kazi ili kufuatilia mienendo ya mabasi kwa urahisi na kuongeza tija na mapato.
“Tukifanya kazi kupitia mifumo ya kielektroniki tunapunguza makosa mengi ya kibinadamu, hivyo matumizi sahihi ya mifumo hii yatatuwezesha kuongeza ufanisi katika utendaji kazi wetu ikiwa ni pamoja na eneo la ukusanyaji wa mapato ya serikali”, amesema Mchengerwa
Aidha, ameagiza DART kudhibiti matumizi mabaya ya njia za mabasi, kutoka kwa njia zilizokusudiwa na kupita njia za mabasi ya Mwendokasi, kusababisha ajali za mara kwa mara.
“Serikali imekua ikitumia fedha nyingi kujenga miundombinu kama mataifa mengine yanavyofanya, wapo watu wako tayari kulipia njia hizo, kama kuna watu wapo tayari kulipia lichakateni tuliweke kwenye kanuni.
Kwa sasa endeleeni kudhibiti.
Pia, Mchengerwa ameagiza kuhimarishwa nidhamu kwa madereva na watoa huduma.
“Kutosimamia nidhamu kwa madereva na watoa huduma, ndio chanzo cha mabasi kugongana, BRT sifa yake ni kuwa salama.