Migogoro binadamu, wanyama kupatiwa dawa
SERIKALI ya Tanzania, imepokea Euro milioni sita, sawa na Sh bilioni 13.2 kutoka Shirika la Ujerumani la GIZ, kwa ajili ya mradi wa kupunguza migogoro baina ya binadamu na wanyamapori hasa kwenye maeneo ya pembezoni mwa hifadhi.
Akizungumza na waandishi wa habari, wakati wa ziara ya kikazi katika Chuo cha Mafunzo ya Maliasili kwa Jamii Likuyu Sekamaganga Wilaya ya Namtumbo, Ruvuma, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja amesema fedha hizo zitatumika kufanya utafiti wa maeneo yenye changamoto za wanyama wakali na waharibifu.
“Mradi huo wa miaka mitatu una lengo la kutoa ujuzi kwa jamii kuhusu namna ya kukabiliana na wanyama wakali na waharibifu, ambapo jamii hizo zitasambaza ujuzi kwa jamii nyinginezo,” alisema waziri Mary.
Amesema mafunzo hayo pia yatatolewa kwa Askari Wanyamapori wa Vijiji (VGS), ili kuongeza nguvu ya kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu.
Alisema kutolewa kwa elimu hiyo itasaidia kuondoa chuki baina ya binadamu na shughuli za uhifadhi, kwani jamii itakuwa na uelewa wa kutosha juu ya uhifadhi na namna ya kukabiliana na wanyama wakali na waharibifu.