Migogoro vyama vya ushirika itatuliwe

KATIBU Tawala wa Mkoa wa Morogoro , Dk Mussa Ali Mussa ametaka migogoro kwenye vyama vya ushirika nchini itatuliwe kwa haraka kwa lengo la kuondoa uzoroteshaji wa majukumu ya vyama hivyo ili kuwezesha uendelevu wa uzalishaji wenye tija.

Dk Mussa amesema hayo Mei 17, 2023 mjini Morogoro wakati anafungua mafunzo ya usimamizi wa vyama vya ushirika katika Kanda ya Mashariki kwa maofisa 78 wa ushirika wa mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro.

Katibu Tawala huyo pia ameitaka Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) ihakikishe inafanya kazi kwa karibu na Mamlaka za Serikali ili kuhakikisha inaboresha maisha ya wananchi kupitia ushirika.

Advertisement

Dk Mussa pia amevitaka vyama vya ushrika vijikite katka kuongeza thamani ya mazao na bidhaa zinazozalishwa ili kujipatia fedha zaidi zikiwemo za kigeni kwa ajili ya kuimarisha uchumi wa nchi na wa vyama vya ushirika.

Naye Naibu Katibu mkuu wa wizara ya Kilimo, Dk Hussein Mohamed Omar amesema udhibiti na usimamizi katika vyama vya ushirika umekuwa mdogo kutokana na maofisa wa ushirika wenye jukumu la kuvisimamia wanakosa uzoefu na ujuzi wa kuviisimamia kwa weledi unaotakiwa.

“ Vyama vya ushirika vimekuwa havikaguliwi kikamilifu kutokana na maafisa kukosa ujuzi wa ukaguzi , na unakosekana kutoka na ukosefu wa mafunzo ya mara kwa mara kwa maafisa hao “ amesema Dk Omar

Dk Omar ametaka mafunzo hayo yakijite katika kutatua changamoto za kiujuzi na kiutendaji kwa maaofisa hao na pia kutaka yatolewe kwa wanachama na viongozi wa vyama vya ushirika kulingana na majukumu yao ili yawe chachu ya mabadiliko katika vyama vya ushirika.