Migogoro ya ardhi Kigoma yakwamisha maendeleo

MKUU wa Wilaya Kigoma, Salum Kali amesema migogoro ya ardhi katika wilaya hiyo imekuwa changamoto  katika utekelezaji mpango wa maendeleo katika wilaya hiyo.

Kutokana na  hali hiyo mkuu wa wilaya huyo alisema kuwa imemlazimua kuandaa kliniki ya ardhi kwa siku tano kuanzia Machi 25 mwaka huu kukutana na wananchi wenye migogoro na kuitafutia ufumbuzi.

Kali alisema hayo kwenye uwanja wa michezo wa Mwanga Community Centre ambapo anaendesha kliniki ya siku mbili kusikiliza kero mbalimbali za wananchi.

Alisema kuwa katika  kliniki maalum ya kusikiliza migogoro ya ardhi atakuwa na  wataalam wote wa idara ya ardhi ya Manispaa ya Kigoma Ujiji na kamishna wa ardhi wa mkoa ili kila jambo lizungumzwe kwa uwazi na kumalizika siku hiyo.

Akizungumza katika kliniki hiyo kwa maalum kusikiliza kero za wananchi wa tarafa ya Kigoma Kaskazini Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji Katibu Tawala wa Wilaya Kigoma, Mganwa Nzota alisema kuwa  jumla ya watu 36 walijitokeza na kati yao 29 walikuwa na kero zinazohusiana na migogoro ya ardhi.

Mwenyekiti wa mtaa wa Kamara kata ya Bangwe Manispaa ya Kigoma Ujiji, Damas Shatiel akizungumza katika kliniki hiyo alisema kuwa migogoro mingi inakuzwa na watu ambao wanafanya mambo yaliyo nje ya taratibu wengi wakiwa hawana nyaraka halali za kumiliki maeneo wanayolalamikia hivyo kumuomba Mkuu wa wilaya Kigoma kutumia vyombo vyake vya ulinzi na usalama kuchunguza,kuwakamata na kuwachukulia hatua.

Shatiel alisema kuwa  watu hao  wamekuwa wakikwamisha michakato mbalimbali ya maendeleo hasa utekelezaji wa miradi ya ujenzi.

Habari Zifananazo

Back to top button