Miili 1,294 yafukuliwa baada ya kuzikwa

KATIKA uchunguzi uliofanywa na Jeshi la Polisi pamoja na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Dar es Salaam, unaonesha kuwa tangu mwaka 2015 hadi 2021, kulikuwa na matukio ya kufukua miili 1,294.

Kati ya matukio hayo, yaliyoruhusiwa kufukuliwa kwa amri ya mahakama ni 52 pekee.

Aidha, Mahakama ya Tanzania imesema ni kosa kisheria kufukua mwili wa marehemu bila kupata amri ya mahakama.

Imesema mhimili huo ndio wenye mamlaka ya kutamka kwamba mwili wa marehemu ufukuliwe kama utakuwa umezikwa au kutozikwa endapo mazingira ya kifo yatakuwa na utata au vifo chini ya uangalizi wa polisi au magereza.

Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, Richard Kabate amesema hayo alipozungumza katika kipindi cha televisheni cha Sema na Mahakama.

Kabate alisema Sheria ya Uchunguzi wa vifo vyenye mashaka kifungu cha 12, kinamtaka yeyote atoe taarifa kwa hakimu mchunguza maiti kuhusu kifo cha mashaka cha ndugu au mtu mwingine.

Alisema baada ya kutoa taarifa hiyo, hakimu ataanzisha kesi na kwa mujibu wa Kifungu cha 6 cha sheria hiyo, atatoa amri ya kufukua maiti kama itakuwa imezikwa au kuamuru marehemu kutozikwa mpaka pale watakapofanya uchunguzi wa kitabibu kubaini sababu za kifo hicho.

Hakimu Kabate alisema wanaofanya uchunguzi wa awali wa mwili wa marehemu, hawaruhusiwi kurudia uchunguzi unaotokana na amri ya mahakama badala yake inaelekezwa kuchaguliwa kwa daktari mwingine ambaye yupo hospitalini hapo au kutoka nje ya hospitali nyingine kufanya uchunguzi.

Alisema askari haruhusiwi kuhusika kwenye uchunguzi bali wakati wa tukio la kufukua mwili ambalo litahusisha wazee wa baraza na hakimu mwenyewe au anaweza kumchagua mtu kushuhudia tukio hilo.

Pia alisema yanapotokea mazingira ya kifo cha utata katika vituo vya polisi au magereza na maeneo mengine, hakimu anaweza kuagiza kufanyika kwa uchunguzi wa kitabibu ambao watatakiwa kujaza fomu namba B na C kueleza sababu za kifo na baada ya majibu wataamua kuzika huku kesi ya msingi ikiendelea dhidi ya mtuhumiwa.

“Kitendo cha kuaga mwili kinachofanywa na Wakristo si kwa bahati mbaya, kipo kisheria na hata Waislamu wanapokwenda kuosha maiti huangalia kuhakiki kama mtu aliyekufa ndiye mwenyewe au la.

“Sababu wapo watu ambao husema fulani amekufa lakini hawakuoneshi mwili wake na huzika tu lazima uwe na mashaka kwanini wanafanya hivyo,” alisema Hakimu Kabate.

Hakimu Kabate alisema mahakama hiyo ni maalumu na inaanzishwa kwa pale tu kuna kifo cha utata na kwamba baada ya kumaliza kesi, haiendelei.

Alifafanua sheria hiyo imerithiwa kutoka Uingereza ambao huanzisha kesi hizo baada ya miezi 12 ya kifo cha marehemu, sheria hiyo haijatamka wazi kama wanaweza kufukua maiti ambayo ni zaidi ya miezi hiyo.

“Katika uchunguzi uliofanywa na Jeshi la Polisi pamoja na Hospitali ya Taifa Muhimbili unaonesha kuwa tangu mwaka 2015 hadi 2021, kulikuwa na matukio ya kufukua mwili 1,294 kati ya hayo yaliyoruhusiwa kufukuliwa kwa amri ya mahakama ni 52 pekee,” alifafanua.

Pia alisema zipo mahakama na mahakimu wa kuchunguza maiti ambao wametamkwa katika Gazeti la Serikali na sheria yake ilianzishwa mwaka 1984.

Hakimu Kabate alisema sheria inaelekeza gharama zote za ufukuaji wa mwili zinatolewa na mfuko wa serikali hivyo jamii haipaswi kugharamia au kukubali kutoa fedha pale watakapoombwa kinyume na sheria.

 

Habari Zifananazo

Back to top button