JESHI la Polisi mkoani Songwe limeokota miili ya wanaume watano katika milima ya Senjele Kata ya Senjele.
Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Theopista Mallya amesema wanaume hao wanakadiriwa kuwa na umri wa miaka 25 hadi 30.
Kamanda Mallya alisema miili hiyo iliokotwa Mei 10 na kuhifadhiwa katika hospitali ya wilaya ya Mbozi, Vwawa na bado haijatambuliwa.
Alisema miili hiyo ilikutwa ikiwa na majeraha maeneo ya kichwani na ameomba wananchi waende kuwatambua marehemu hao.
“Mpaka sasa hakuna mwili ambao umetambuliwa na ndugu pamoja na baadhi ya watu kufika hospitalini kwa ajili ya kutambua miili ya marehemu, niwakumbushe ndugu ambao hawajawaona vijana wao siku za hivi karibuni…,” alisema Kamanda Mallya.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Mbozi, Dk Keneth Lesilwa alisema Mei 10, mwaka huu saa saba mchana polisi waliwapelekea miili mitano ya wanaume.
Dk Lesilwa alisema marehemu hao hawana majeraha makubwa ila wana michubuko sehemu za usoni na wamevimba vichwa na uchunguzi zaidi unaendelea.
“Mpaka sasa ni watu wachache wamefika hospitalini kwa ajili ya utambuzi lakini hakuna aliyetambulika. Nawashauri ndugu na jamaa wafike hospitali kuwatambua marehemu, kabla utaratibu mwingine wa halmashauri haujachukuliwa ikiwa watakaa hospitalini hapo kwa muda wa zaidi ya wiki moja,” alisema.
Taarifa zinadai kuwa huenda watu hao waliuawa usiku wa kuamkia Mei 10, mwaka huu na huenda hawakuuawa katika eneo walipokutwa.
Miili hiyo ilikutwa imetupwa kandokando ya milima ya Senjele katika Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe.