MWANZA: WADAU wa usalama barabarani wameishauri Tanzania kutekeleza ipasavyo,sera ya taifa ya usalama barabarani na mpango kazi, ili kufikia lengo la ajali sifuri.
Wametoa wito huo leo Novemba 27, 2023 wakati wa semina ya wiki moja ya usalama barabarani iliyowakutanisha wadau kutoka nchi mbalimbali za Afrika na nje ya Afrika, kujadili mikakati ya kukomesha ajali Tanzania na bara la Afrika kwa ujumla.
Mshiriki kutoka nchini Uganda, Jemima Nalumansi, amesema utekelezaji wa mpango huo uhusishe programu zinazohimiza uboreshaji wa miundombinu ya barabara, utekelezaji thabiti wa sheria za usalama barabarani, kutilia mkazo kampeni za elimu kwa umma, pamoja na huduma za matibabu ya dharura.
“Nchini kwetu tunatekeleza mkakati huu ipasavyo na tunafanikiwa kuthibiti ajali kwa kiasi kikubwa, ingawaje kwa hapa sina takwimu kamili,” amesema.
Akizindua semina hiyo, Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Ndani, Jumanne Sagini, amesema lengo la kukutana na wadau hao wa kimataifa ni kubadilishana ujuzi na maarifa, yatakayoisaidia Tanzania kufikia lengo, kwani kwa sasa ajali zinagharimu maisha ya watu zaidi ya 15,000 nchini, kwa mwaka.“Hii ni kwa mijibu wa takwimu za shirika la afya duniani,” amesema.
Comments are closed.