Kilimo umwagiliaji kukabili mabadiliko tabianchi

KIASI cha Sh milioni 450 kimetumika ili kufanikisha majaribio ya kilimo cha umwagiliaji katika mikoa ya Manyara,Iringa, Dodoma,Songwe na Njombe ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya kuboresha mifumo ya masoko ya kilimo Tanzania (AMDT), Charles Ogutu alisema kiasi cha fedha kilichotengwa ni Sh milioni 600 huku wakitarajia kwenda mikoa mingine zaidi.

Advertisement

“Kazi kubwa tunayofanya ni kuhakikisha mkulima yoyote azingatie mabadiliko ya tabianchi anapotaka kulima azingatie zile taarifa ,teknolojia na mbinu mpya ambazo zinaweza kumsaidia asipoteze mazao,”ameeleza.

Ameongeza “Hili linajumuisha mfano kutumia mbegu ambazo ni stahimilivu na za muda mfupi lakini pia kutumia mbinu mbalimbali hasa zile zinazohifadhi maji badala ya kupoteza.

Ogutu ameeleza kuwa mazao yanayozalishwa yanasaidia sana taifa  huku akitolea mfano wa mazao kama maharage ni ya muda mfupi inasaidia kwenye usalama wa chakula kwani usalama wa chakula ni wa taifa na chakula ikikosekana ni hatari.

“Mazao yote ambayo tunashughulika nayo ni yale yanayotumika kwa chakula nchini tumewahi kuwa na mradi wa zao la mahindi, alizeti kuhakikisha taifa linajitosheleza  bila kutegemea nje,”amebainisha.

Amesema wakulima lazima watambue kutumia mbinu na namna mbalimbali kuhakikisha wanatumia mbinu za kisasa (Climate Smart Practises) ikiwemo kuchimba mashimo ambayo yatahifadhi maji ambayo siyo ya kung’oa kila kitu badala yake kubakizwa shambani.

“Kwanza niseme hivi hakuna zao linalohitaji mvua mazao yote yanahitaji unyevu hata maji yanaleta unyevu wakulima wakikaa kutegemea mvua watapata hasara au wanaweza kuvuna mvua ikija kwa wakati na kiasi tegemewa.

Amesisitiza kuwa wanawahamasisha wakulima ni namna gani wanaweza kutumia maji yaliyopo ambayo yanaweza kuwa ya visima,miti,maziwa wayatumie  kwa namna ambayo wataweza kuzalisha.

Ogutu amesema wanapeleka elimu kupitia wadau ili wakulima wajue  na inawasaidia ili kama kuna maji wanaweza kulima mara mbili hata mara tatu kwa mwaka kwasababu mazao mengi wanayolima wakulima yanaweza kustawi ndani ya siku 90 hadi 120.

“Baada ya hapo wanaweza kubadilisha kama alipanda maharage anapanda mahindi ukitoa hata zao lingine watakuwa wameongeza kipato na wanatumia mbinu ya kurutubisha shamba lisichoke sana.

Aidha amesema licha ya elimu na taarifa wameweza kusaidia wakulima kuona teknolojia wakazitumia ikiwemo umwagiliaji kwa njia ya matone  na  baadhi ya wakulima wamechimba visima wenyewe na tayari wameanza kuona mabadiliko.

Pia ameeleza kuwa wanawezesha taasisi za tafiti waweze kuzalisha mbegu ambazo zinaweza kustahimili mabadiliko ya tabianchi na ziweze kuwafikia wakulima.

“Kilimo cha umwagiliaji ni kumfikishia maji alipo badala ya kusubiri mvua hata kama hayupo karibu na mito wanatumia njia ya kumwagilia kwa kujenga njia na drip irrigation ni matone na kunanjia ya kupuliza kutoka juu,”amefafanua.

Kwa upande wake wakulima wa alizeti katika Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma wameeleza namna kilimo cha umwagiliaji kinavyowanufaisha wakati huu wa mabadiliko ya tabianchi.

Katibu wa Kikundi cha Umoja wa Umwagiliaji Mkoka ,Oznieli Abednego amesema kabla ya kuingia kwenye kilimo hicho mavuno yalikuwa hayaridhishi kwani wakuliwa wanapata gunia tatu hadi tano za alizeti na sasa wamefanikiwa kuvuna magunia 75.

“Tulilima shamba ekari 25 na kwa sasa tutalima mara mbili kwa mwaka kwani hatutegemei tena kilimo cha msimu wa mvua.

Amesema kupitia kilimo cha umwagiliaji kikundi kimeweza kununua trekta ,guta na maisha ya wanakikundi yamebadilika na mwitikio wa watu kujiunga umezidi kuwa mkubwa.

Habari imewezeshwa  na MESHA na Ofisi ya Afrika ya IDRC Mashariki na Kusini.

 

11 comments

Comments are closed.