Mikataba 10 yasainiwa kuzalisha ajira 16,355

KITUO cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimeingia mikataba na kampuni 10 ya uwekezaji wa kimkakati mahiri yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 1.8.

Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Ashatu Kijaji alishuhudia utiaji saini mikataba ya uwekezaji huo uliopewa hadhi na Kamati ya Taifa ya Uwekezaji (NISC).

Unatajwa kuwa ni wa kwanza kushuhudiwa na Kituo cha Uwekezaji (TIC) na utatoa ajira za moja kwa moja 16,355 na ajira zisizokuwa za moja kwa moja 200,000.

Akizungumza wakati wa utiaji wa saini wa mikataba hiyo, Kijaji alizitaka taasisi hizo kupunguza na kumaliza changamoto ya Tanzania kuagiza bidhaa kutoka nje wakati uwezo wa kuzalisha upo nchini.

Alisema serikali imekuwa ikiongeza nguvu kwa wakulima, ili waweze kuzalisha malighafi za kutosha zitakazoweza kuchakatwa na viwanda vya nchini na kuzalisha bidhaa zitakazouzwa ndani na nje ya nchi. Kijaji alisema nchi itaondokana na uagizaji wa sukari mwaka 2024.

Alizitaka kampuni za kuchakata mafuta kumaliza kilio cha Watanzania kuhusu uhaba wa mafuta ya kupikia ifikapo mwaka 2027 kwa kuzalisha mafuta tani 560,500 kutoka tani 205,000 zinazozalishwa sasa.

“Haina haja ya kuagiza mafuta kutoka nje, wakati wapo wakulima ambao wanalima mbegu za kukamua mafuta. Kilio cha wawekezaji ilikuwa ni kuwepo kwa viwanda lakini wanakosa malighafi, kwa sasa serikali imewekeza huko tukafanye kazi,” alisema.

Aliongeza kwa kusema serikali itazindua mtandao wa kituo kimoja kwa ajili ya mwekezaji kupata huduma zote sehemu moja, ili kumpunguzia usumbufu wa kutembea na nyaraka kutafuta cheti.

Alisema huduma hiyo itasaidia wageni kuomba vibali na kukamilika kwa siku tatu na haitakuwa na usumbufu kama ambao ulikuwa ukijitokeza mwanzo kutokana na utofauti wa kanuni na kisheria na kufanya baadhi ya wawekezaji kushindwa kuwekeza.

“Nitaendelea kuwaambia kwamba Tanzania si kisiwa kama tupo peke yetu, mwekezaji ukimsumbua anafanya kujadili na kwenda nchi nyingine,” alisema.

Katika kampuni hizo 10 zilizosaini mkataba, sita ni za nje ya Tanzania, tatu ni za wazawa na moja ina ubia na sekta binafsi. Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Gilead Teri alisema tangu kuanzishwa kwa kituo hicho, kwa mara ya kwanza kimeshuhudia utiaji wa saini wa mikataba ya utekelezaji na kampuni 10 kwa wakati mmoja.

Alisema mikataba hiyo inaashiria mafanikio makubwa ya kipindi cha uboreshaji wa mazingira ya uwekezaji, kuongezeka kwa ufanisi wa utoaji wa huduma kwa wawekezaji na kuimarika kwa juhudi za uhamasishaji uwekezaji nchini.

“Tunashukuru wawekezaji walioamua kuungana na juhudi za serikali kuwaletea wananchi maendeleo na kukuza uchumi kupitia uwekezaji,” alisema.

Habari Zifananazo

1 Comment
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button