Mikoa 14 yaagizwa kuhifadhi chakula

MIKOA 14 pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba itakuwa na mvua za vuli chini ya wastani hivyo wananchi wametakiwa kupanda mazao yanayokomaa kwa muda mfupi na kutunza chakula.

Kutokana na upungufu huo wa mvua za vuli mwaka huu, wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya wanatakiwa kutoa taarifa za hali ya hewa kama sheria za usimamizi wa maafa zinavyowataka kufanya.

Akizungumza jijini hapa jana, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), George Simbachawene alisema kutokana na utabiri wa hali ya hewa, maeneo mengi nchini ambayo mara nyingi huwa yanapata mvua za vuli za kutosha katika kipindi cha Oktoba hadi Desemba, hayatapata za kutosha.

“Taarifa ya utabiri huu inahusu maeneo yanayopata mvua misimu miwili kwa mwaka, mvua zinatarajiwa kuwa chini ya wastani hadi wastani katika maeneo mengi ya mikoa mbalimbali pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba,” alisema.

Mikoa itakayokuwa na upungufu wa mvua za vuli ni pamoja na Kagera, Geita, Mwanza, Mara, Shinyanga, Simiyu, Kigoma, Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Tanga, Dar es Salaam, Pwani, Morogoro na visiwa vya Unguja na Pemba.

Simbachawene alisema pamoja na uchache wa mvua hizo, pia zitaanza kwa kuchelewa, zikiwa na mtawanyiko usioridhisha na kuambatana na vipindi virefu vya ukavu.

Mvua hizo zilianza wiki ya nne ya Septemba katika ukanda wa Ziwa Victoria na zitaanza wiki ya nne ya Oktoba maeneo ya Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki.

Ongezeko la mvua katika maeneo mengi linatarajiwa Desemba na kumalizika Januari mwakani.

Alisema vilevile kina cha maji katika mito, mabwawa na hifadhi ya maji ardhi kinatarajiwa kupungua hususani katika maeneo yanayotegemea mvua za vuli, hivyo kusababisha upungufu wa maji katika matumizi mbalimbali.

Kunaweza kujitokeza milipuko ya magonjwa kutokana na upungufu wa upatikanaji wa maji safi na salama katika maeneo mbalimbali.

Katika kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na upungufu wa mvua hiyo, Simbachawene aliziagiza Kamati za Usimamizi wa Maafa katika ngazi ya mkoa hadi vijiji na mitaa ziwajibike katika kutekeleza mambo saba katika sekta za kilimo, maji, afya, mifugo, miundombinu na nishati.

Kutokana na upungufu wa mvua za vuli nchini, Ofisi ya Waziri Mkuu imetoa maelekezo kwa Kamati za Usimamizi wa Maafa za mikoa, wilaya, kata, vijiji na  mitaa ambazo zina jukumu la usimamizi wa maafa, kuchukua hatua mara moja ikiwa ni pamoja na kuandaa mpango wa dharura itakayoelekeza hatua za kuchukua kwa kila taasisi na wananchi.

Habari Zifananazo

Back to top button