Mikoa 5 yakithiri ukataji miti
MIKOA mitano imetajwa kuwa vinara wa ukataji miti hovyo na kuharibu vyanzo vya maji.
Mikoa hiyo iliyotajwa kuharibu misitu na miti asili kwa kiasi kikubwa, Pwani, Morogoro, Tabora, Lindi na Ruvuma.
Akizungumza leo Novemba Mosi, 2022 Rais Samia Suluhu Hassa, amesema mabadiliko ya tabia nchi yana sura mbili, ambazo moja ni sura ya kimungu, lakini sura ya pili ni ya kibinadamu ambao ndio chanzo kikuu cha uchafuzi wa mazingira na uharibifu mkubwa wa vyanzo vya maji.
“Upungufu wa maji Dar es Salaam chanzo kikuu ni Mkoa wa Pwani, wanakata sana miti hovyo na ndio wapo karibu na mto Ruvu,” amesema Rais Samia na kuongeza:
“Vyanzo vya maji vinapungua, watu wanaolima wanablock maji yanashindwa kuflow, tena mashamba yenyewe ni ya wageni, watu wamejenga mabwawa wanafuga samaki wanazuia maji, ujenzi holela ndani ya Jiji la Dar es Salaam, na mifumo iliyopo ndio chanzo cha kuziba kwa vyanzo vya maji.
“Hivyo, naiagiza Dawasa, Mkuu wa Mkoa mmefanya operesheni kwa wale wote waliokuwa wanazuia maji, lakini hiyo pekee haitoshi, nataka mkasafishe mto, maji yapatikane.
“Namtaka Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa), akahakikishe maagizo ya kuunganisha maji kutoka Kigamboni lita milioni 70 zimekamilika, fedha zilishatolewa nataka kuona flow ya maji yanaingia Dar es Salaam kupunguza upungufu wa maji,” amesema.
Amesema ujenzi wa Bwawa la Kidunda, mkataba umesainiwa jana, na kukamilika kwake ni miaka miwili na kujaa kwake ni mvua kunyesha, lakini ndani ya miaka mitano Dar es Salaam itaondokana na upungufu wa maji.