BUNGE limepitisha na kuridhia Azimio la serikali la kufuta Hifadhi ya Taifa Kigosi ili kuruhusu kuanzishwa kwa Hifadhi ya Msitu Kigosi, itakayosimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).
Akiwasilisha Azimio hilo bungeni Dodoma jana, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mohammed Mchengerwa alisema baada ya kuanzishwa kwa Hifadhi ya Kigosi eneo hilo lilisimamiwa na Sheria ya Hifadhi za Taifa Sura 282 inayozuia kufanyika kwa shughuli za kibinadamu ukiwemo ufugaji nyuki, uvuvi wa samaki na shughuli za kimila.
Mchengerwa alitaja manufaa ya kufutwa kwa hifadhi hiyo kuwa ni kuanzishwa kwa Hifadhi ya Msitu Kigosi yenye ukubwa wa kilometa za mraba 7,460 itakayosimamiwa na Sheria ya Misitu, Sura ya 323.
Alieleza kuwa hifadhi hiyo itakuwa na manufaa ya kiuchumi kwa wananchi wa mikoa mitano ya Geita, Kagera, Kigoma, Shinyanga na Tabora; wilaya sita za Bukombe, Mbongwe, Biharamulo, Kakonko, Kahama, Kaliua na kata 25.
Aidha, Mchengerwa alisema vijiji 126, kaya 113,547 zitanufaika na uamuzi huo. “Wananchi wataruhusiwa kufanya shughuli za kiuchumi ndani ya hifadhi hiyo ukiwemo ufugaji nyuki na uvuvi wa samaki kwa mujibu wa sheria.
Kuchochea shughuli za ufugaji nyuki kibiashara ambapo wafugaji 1,764 wenye mizinga zaidi ya 521,406 waliokuwepo awali kwenye maeneo hayo wataongezeka maradufu,” alieleza Mchengerwa. Alisema hatua hiyo itachangia ongezeko la uzalishaji wa asali nchini kutoka wastani wa tani 32,691 hadi 138,000 kwa mwaka na kuongeza mauzo ya mazao nyuki nje ya nchi.
Pia, alisema hifadhi hiyo ya msitu itatoa uhakika wa malighafi kwa viwanda sita vya kuchakata na kufungasha mazao ya nyuki ambavyo ujenzi wake umewezeshwa na serikali kwa zaidi ya gharama ya Sh bilioni 2.5 kwenye wilaya za Mlele, Kibondo, Bukombe, Nzega, Sikonge na Manyoni. Aidha, Mchengerwa alisema katika msitu huo shughuli za kimila zitaruhusiwa kufanyika na hivyo kujenga mahusiano mema kati ya wananchi na wahifadhi kupitia programu ya usimamizi shirikishi wa misitu kwa mujibu wa Sera ya Taifa ya Misitu ya Mwaka 1998.
Faida na fursa nyingine alizotaja ni kuongeza mchango wa sekta ya misitu na nyuki katika Pato la Taifa. Mchengerwa alisema kwa mujibu wa masharti ya nyongeza ya kifungu cha 4 cha Sheria ya Hifadhi za Taifa, Sura ya 282, Rais amepewa mamlaka ya kurekebisha mipaka ya eneo lolote lililotangazwa kuwa Hifadhi ya Taifa baada ya kupata idhini ya Bunge na kwa tamko litakalochapishwa kwenye Gazeti la Serikali.
Aidha, alisema Rais ameridhia kufutwa kwa Hifadhi ya Taifa Kigosi na kuanzishwa kwa Hifadhi ya Msitu Kigosi kutokana na manufaa hayo ya kiuchumi, kijamii na kimazingira.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Najma Giga alishauri wananchi na wawakilishi wao waelimishwe na kushirikishwa katika michakato ya kubadili mipaka au matumizi ya maeneo ili wawe na uelewa wa pamoja kuhusu dhamira ya serikali na mantiki ya michakato hiyo.
Pia, kamati hiyo iliishauri TFS iimarishe ulinzi katika msitu huo kwa kuwa wananchi wataruhusiwa kufanya shughuli za kiuchumi ili wanyama wakali na waharibifu kama vile simba, chui na viboko wasisababishe madhara.
Comments are closed.