Wajumbe 900 kujadili ukeketaji Afrika
DAR ES SALAAM: WASHIRIKI 900 kutoka nchi mbalimbali za Umoja wa Afrika wanatarajiwa kuhudhuria mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Kutokomeza Ukeketaji ambao umepangwa kufanyika Oktoba 9 hadi 11,2023 Jijini Dar es salaam.
Katika Mkutano huo Tanzania itakuwa na washiriki 200 na Nchi nyingine wanachama wa Umoja wa Afrika na Mabara mengine watakuja washiriki 700.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Waziri wa Maendeleo ya Jamii,Jinsi,Wanawake na Makundi Maalumu,Dk Doroth Gwajima amesema Washiriki wa ndani watatoka Mikoa mbalimbali hasa ile yenye takwimu za juu za ukeketaji kwa kuwa wanao uzoefu wa kutosha katika utekelezaji wa afua za kutokomeza vitendo vya ukeketaji.
Amesema kwa mujibu wa takwimu za Afya, Idadi Watu na Viashiria vya Malaria za mwaka 2015/16 zinaonyesha kwamba ukeketaji umepungua kutoka asilimia 30 mwaka 2010 hadi asilimia 10 mwaka 2015 na kuna baadhi ya Mikoa takwimu zake ni za juu zaidi ya wastani.
Ameitaja Mikoa hiyo kuwa ni Manyara asilimia 58, Dodoma asilimia 4, Arusha asilimia 41, Mara asilimia 32, Singida asilimia 31 na Tanga asilimia 14.
“Katika kukabiliana na mila na desturi ya ukeketaji, Serikali imekuwa ikishirikiana na Wadau wa Maendeleo kufanya tafiti ili kubaini ukubwa wa tatizo na kupendekeza hatua za kuchukua kukabiliana na changamoto hiyo.
“Baadhi ya afua zinazotekelezwa na Serikali ni pamoja na kutunga Sheria Kanuni ya adhabu kifungu 169A na Sheria ya Mtoto Na. 21 ya mwaka 2009 na kutoa elimu kwa makundi mbalimbali ya jamii kuhusu madhara ya ukeketaji ili waachane na mila hiyo,”ameeleza.
Dk Gwajima amesema lengo ni kutoa fursa kwa wadau wanaopambana na ukeketaji kuunganisha nguvu za pamoja, kubadilisha uzoefu, kujengeana uelewa na maarifa katika kuimarisha mapambano ya kutokomeza vitendo vya ukeketaji katika nchi za Afrika.
Pia amebainisha kuwa mkutano huo ni sehemu ya utekelezaji wa Ajenda ya Maendeleo Endelevu ya mwaka 2030 na Agenda ya 2063 ambazo zote mbili zimeweka ajenda ya kutokomeza ukeketaji na aina zote za mila na desturi zenye madhara kwa wanawake na wasichana kuwa kipaumbele muhimu na vinahitaji kufanyiwa kazi haraka.
kaulimbiu ni “Mabadiliko katika kizazi kimoja kwenda kingine ni muhimu katika kutokomeza vitendo vya ukeketaji”