Mikopo kumaliza changamoto TAMONGSCO

SHIRIKISHO la Wamiliki na Mameneja wa Shule na Vyuo Visivyo vya Serikali (TAMONGSCO) limeiomba Kamati ya Bunge ya Elimu pamoja na Taasisi za Kifedha kuangalia namna bora ya kupata mikopo yenye riba nafuu kwa ajili ya kukabiliana na changamoto zao.

Akizungumza kwenye mkutano wa mwaka uliofanyika Dar es Salaam leo Juni 15, 2023 mgeni rasmi, Waziri wa zamani wa Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka amesema TAMONGSCO inakabiliana na changamoto ya vitendea kazi, pamoja na walimu.

Advertisement

Tibaijuka amesema kwa kutambua juhudi za serikali katika sekta ya elimu, ila TAMONGSCO imekuwa na changamoto hizo kutokana na gharama za vifaa vya kufundishia kuwa juu.

“Serikali haiwezi kumaliza mambo yote, ndio maana TAMONGSCO tupo hapa kupunguza presha kubwa ambayo ingekuwa serikalini.” amesema Prof Tibaijuka.

Prof Tibaijuka amesema baadhi ya waendeshaji wa shule hizo kwasasa wanatoa huduma kwa hasara kutokana na hali ngumu ya kifedha, na kuwa kama hisani tu.

Tibaijuka ambaye pia ni miongoni mwa wamiliki wa shule amegusia changamoto ya elimu maeneo ya vijijini ambapo amesema licha ya Rais Samia kujizatiti kwenye ujenzi wa shule ila baadhi ya maeneo bado yana changamoto ikiwemo Jimbo la Muleba hasa katika kipindi chake akiwa bungeni.

“Hali halisi maeneo ya Muleba sio nzuri, wapo wanafunzi wanaosomea chini miti.” ameongeza Prof Tibaijuka.

Mwenyekiti wa TAMONGSCO, Alfred Luvanda amesema lengo la kuomba mikopo hiyo ni kuwekeza kwenye maabara kwa kupata, kompyuta na vifaa vingine vya kufundishia elimu ya sayansi.

Amesema serikali inapaswa kuwawezesha wamiliki wa shule na vyuo hivyo kwa lengo la kutoa elimu bora na kwa kushirikiana na serikali yenyewe.

Aidha, Mkurugenzi wa Kampuni ya Tanzanite, Elina Mwangomo ambao ndio waandaaji wa tukio hilo amewaomba wadau kujitokeza kwa ajili ya huduma ya kuandaa matukio ya aina hiyo.