SERIKALI ya Korea Kusini kupitia Taasisi ya Takwimu (KOSTAT) imetumia Sh milioni 120 kuboresha kituo cha kuchakata takwimu nchini.
Kamisaa wa Sensa Tanzania Bara, Anne Makinda alisema kituo hicho cha kupokea na kuchakata takwimu kitakuwa chanzo muhimu cha kuongeza maarifa.
Makinda alisema hayo Dodoma jana wakati wa kufunga mwaka wa pili wa mradi wa ushirikiano baina ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na KOSTAT.
“Kituo hiki cha mafunzo ni alama iliyoanzishwa kupitia mradi wa ushirikiano baina ya NBS na KOSTAT katika mwaka wake wa pili kati ya miaka mitatu (2021-23). Kituo hiki ni matokeo muhimu ya maarifa katika kuifaidisha wanufaika,” alisema.
Makinda alisema ushirikiano katika mradi huo pia ulijikita katika kujengea uwezo wataalamu NBS kwa kuwapa mafunzo ndani ya nchi na nchini Korea Kusini.
Mradi huo pia umesaidia kutoa kompyuta 600 kwa ajili ya upimaji ramani na utengaji wa maeneo kwa ajili ya maandalizi ya sensa ya watu na makazi iliyofanyika Agosti 23, mwaka huu.
Wakati miaka miwili ya utekelezaji wa mradi ikimalizika, tayari chumba kitakachotumika kama kituo cha kukusanya na kuchakata takwimu kikiwa na vifaa vya kisasa kimekamilika na kinafungua ukurasa mpya wa maendeleo ya miundombinu ya ukusanyaji takwimu nchini.
Mkurugenzi wa KOSTAT Korea Kusini, Hae Ryun Kim alisema mradi huo wa ushirikiano 2021-23 unatarajiwa kutumia Sh bilioni nne na utaendeleza ushirikiano zaidi katika kuimarisha uwezo wa NBS katika kuchakata takwimu bora na kwa wakati.
Kim alisema katika mwaka wa mwisho wa mradi huo 2023, KOSTAT inalenga kuendelea kuboresha kituo cha kuchakata takwimu kutoka taasisi nyingine pia kwa matumizi na manufaa ya nchi na kimataifa.
Mratibu wa Mradi wa Ushirikiano NBS Tanzania, Deogratius Malamsha alisema katika mwaka wa tatu mradi huo utajikita kuimarisha ukusanyaji takwimu kutoka taasisi nyingine za umma na binafsi na kuzichakata katika kituo hicho NBS.
Mratibu wa Utekelezaji wa Mradi kupitia KOSTAT, Charlie Seo alipongeza ushirikiano aliopata NBS wakati wa uboreshaji chumba cha kukusanya na kuchakata takwimu.