Mil.20 wamenufaika huduma madaktari kutoka China

KIGOMA: Watanzania milioni 20 wamenufaika na huduma za matibabu ya kibingwa kutoka kwa madaktari Bingwa kutoka China ambao wamekuwa wakiendesha kambi mbalimbali za matibabu nchini.

Balozi wa China nchini Tanzania,Chen Mingjian alisema hayo wakati wa uzinduzi wa kambi ya madaktari bingwa katika jimbo la Kigoma Kaskazini, mkoani Kigoma, ambapo madaktari bingwa 11 kutoka China watatoa huduma za ushauri na upasuaji kwa wananchi wa jimbo hilo kwa siku tano.


Balozi huyo alisema kuwa kambi hizo za madaktari bingwa ni sehemu ya uhusiano ulioanzishwa na waasisi wa mataifa hayo ulioanza mwaka 1964, ambapo mwaka 1968 China ilianza kutuma madaktari Tanzania na tayari wagonjwa milioni 20 wamepatiwa matibabu na madaktari hao kwa safari 26 walizofanya Tanzania Bara na safari 32 kwa Zanzibar.

Awali akizungumza katika uzinduzi huo Mbunge wa jimbo la Kigoma Kaskazini, Wilaya ya Kigoma mkoani Kigoma, Asa Makanika alisema kuwa ujio wa madaktari hao unatokana na mahitaji makubwa ya huduma hiyo kutokana na idadi kubwa ya watu wa jimbo hilo kushindwa kumudu gharama za matibabu ya kibingwa.

Makanika alisema kuwa pamoja na kazi kubwa inayofanywa na serikali kuimarisha na kuboresha huduma za afya mkoani humo, lakini bado huduma za madaktari bingwa zimekuwa changamoto kubwa kutokana na kutowepo kwa idadi ya kutosha ya madaktari bingwa mkoani humo.

Mganga Mkuu wa Mkoa Kigoma, Dk. Jesca Leba ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa Kigoma,Thobias Andengenye kwenye uzinduzi huo, alisema kuwa Mkoa Kigoma unakabiliwa na upungufu wa asilimia 60 wa watoa huduma za afya na vifaa vya matibabu na upatikanaji wa huduma ya madaktari bingwa ni changamoto kubwa mkoani humo.

Ujio wa madaktari hao 11 utawezesha wananchi wasiopungua 1500 kupata huduma mbalimbali ,ikiwemo huduma za upasuaji,dawa na vifaa tiba vingine bila malipo katika vituo vya Bitale na Simbo kuanzia Oktoba 15 hadi 20 mwaka huu.

Habari Zifananazo

Back to top button