‘Mimba, ndoa za utotoni bado changamoto’
LICHA ya takwimu zilizotolewa Mei 25, 2022 kuonesha idadi ya wanafunzi walioacha shule kutokana na mimba kupungua kwa asilimia 12.8 hapa nchini, lakini bado Tanzania inatajwa kuwa na kiwango cha juu cha mimba za utotoni na ndoa za utotoni.
Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Canada, Helen Fytche alisema hayo jana Mkuranga mkoani Pwani, katika hafla ya kukabidhi vifaa mbalimbali kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum iliyoandaliwa na Shirika lisilo la Kiserikali la HakiElimu.
Katika hafla hiyo HakiElimu imetoa msaada wa sare na vifaa vya shule vyenye thamani ya Sh milioni 60 kwa wanafunzi wa kike zaidi ya 280 wanaotoka katika familia duni, ili kuwawezesha kuendelea na masomo yao ya sekondari bila vikwazo.
Msaada huo ni moja ya matokeo ya mradi wa kupunguza mdondoko na kuongeza ufaulu kwa watoto wa kike (Girls Retention and Transition Initiative), unaofadhiliwa na Serikali ya Canada.
Akizungumza Hellen amesema suala la elimu, Canada inaamini katika kutoa fursa sawa na kupata elimu bora kwa wasichana kama njia bora ya kuondosha vikwazo kwa wanawake na wasichana kijamii, kiuchumi na kisiasa kwa kuboresha fursa
Amesema mabinti wa Kitanzania wanakabiliwa na changamoto nyingi kupata elimu salama, yenye ubora na kuzingatia jinsia.
“Mimba za utotoni, ndoa za utotoni, ukatili wa kijinsia, kazi za nyumbani na ukosefu wa bidhaa na mazingira duni ya kujistiri wakati wa hedhi shuleni ni changamoto katika mahudhurio shuleni,” amesema.
Naye Mkurugenzi Mtendaji HakiElimu Dk John Kalage amesema mradi huo wa miaka mitatu unafadhiliwa na serikali ya Canada na unatekelezwa katika jumla ya shule 67, ambapo shule 34 ni za Msingi na 33 Sekondari, katika wilaya 12 za Tanzania Bara ambazo ni Masasi, Kilwa, Mkuranga, Tunduru, Arusha, Babati, Bariadi, Tabora, Ukerewe, Serengeti, Geita na Sumbawanga.
Amesema kwa kushirikiana na watalaamu mbalimbali katika ngazi ya wilaya, mradi huo umewezesha utolewaji wa mafunzo ya kijinsia na ulinzi wa mtoto, utengenezaji wa sodo, uanzishaji wa madawati ya kuzuia ukatili shuleni na ugawaji wa vyerehani kwa ajili ya elimu ya ufundi na ushonaji wa sodo vyenye thamani ya sh milioni 57.
Amesema kazi kubwa iliyofanyika kupitia mradi huo ni pamoja na kuboresha miundombinu ya shule yenye thamani ya takribani Sh milioni 330 kwa kujenga vyoo vyenye vyumba maalumu vya kujisitiri kwa ajili ya wasichana, ujenzi wa hosteli kwa wasichana na ujenzi wa visima vya maji shuleni.
Amesema suala la kutoa msaada wa sare na vifaa vya shule limefanyika kwa miaka miwili mfululizo, ambapo mpaka sasa jumla ya wasichana 544 wamenufaika na msaada huo.
“Kwa kuwa wasichana hawa wanatoka maeneo tofauti na kwa kuzingatia sababu mbalimbali, HakiElimu imeamua kufanya hafla fupi ya kuzindua ugawaji wa sare na vifaa vya shule kitaifa katika shule ya sekondari Dundani iliyopo Wilaya ya Mkuranga, ambayo ni shule mojawapo ya mradi,” amesema.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Khadija Nassir ametoa wito kwa mashirika yasiyo ya kiserikali na wadau wa maendeleo kushirikiana na serikali kuhakikisha mtoto wa kiume nae analindwa dhidi ya vitendo vya ukatili sawa na mtoto wa kike.
Khadija pia ameishukuru HakiElimu kuchagua Wilaya ya Mkuranga kuwa miongoni mwa Wilaya 12 zinazonufaika na mradi wa kupunguza mdondoko na kuongeza ufaulu kwa watoto wa kike unaofadhiliwa na Serikali ya Canada.
“Wakati tunaendelea kuangalia namna ya kuwanusuru watoto wakike dhidi ya ukatili, pia tutambue watoto wetu wa kiume hawapo salama sana kwenye janga hili la ukatili kwani kumekuwa na matukio ya ulawiti kwa watoto hawa,” amesema.