Minara 2,600 kumaliza tatizo la mawasiliano
WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amelieleza Bunge kuwa sasa serikali ipo kwenye mchakato wa kutafuta fedha za ujenzi wa minara zaidi ya 2,600 ili kumaliza tatizo la mawasiliano kwenye maeneo mbalimbali nchini.
Nape alitoa kauli hiyo bungeni jana alipokuwa akitoa ufafanuzi wa maswali ya wabunge baada ya Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson, kusema nchi imefikia hatua ya kupanua mawasiliano Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) wakati maeneo mengine bado hayana.
Waziri Nape alisema suala la mawasiliano sasa litafika mwisho kutokana na mradi huo. Aliwaomba wabunge wavumilie kwa kuwa michakato inaendelea vizuri.
“Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kumuunganisha kila Mtanzania alipo, mradi huu ukikamilika hili litakwisha, lakini kuna mradi wa minara zaidi ya 100 imejengwa haijawashwa kwa kuwa wakati inajengwa, kulitokea tatizo la virusi vya corona na hivyo kusababisha vipuri vingine kutokuja lakini sasa vipo nchini na hivi karibuni minara itawashwa,” alisema.
Aliongeza: “Bunge lilipitisha bajeti hapa la ujenzi wa minara zaidi ya 728 ambayo zabuni yake imetangazwa Oktoba 20, mwaka huu na inafunguliwa Desemba 20, mwaka huu, najua watu walitamani baada ya bajeti ujenzi uanze lakini kuna mchakato wa kutangaza zabuni na kupata wakandarasi, wabunge wengi maeneo yenu yatafikiwa.”