Mipaka isiyo rasmi Kagera changamoto udhibiti Ebola
CHANGAMOTO ya mipaka isiyo rasmi zaidi ya 1,000 katika Mkoa wa Kagera, inaiweka rehani Tanzania kupata mlipuko wà ugonjwa wa Ebola.
Kagera ambayo inapakana na nchi nne za Uganda, Rwanda, Sudan Kusini upande wa Juba na Kenya upande wa Kisumu imeelezwa kuwa na hatari kubwa ya kupata Ebola, kutokana na mwingiliano mkubwa wa kazi za kiuchumi kwenye mipaka rasmi na isiyo rasmi.
“Naiona hatari kubwa kwa Kagera kutokana na kuingiliana karibu sana na Uganda, Uganda mpaka sasa wana wagonjwa 43 na jumla ya vifo 29 tusiogope, “amesema Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu na kuongeza:
“Kinachotunyima usingizi ni ugonjwa huu mbaya, vifo ni asilimia 40 na inategemea na aina ya matibabu, lazima tuelezane ukweli mipaka rasmi ni saba, mipaka isiyo rasmi ni zaidi ya 1,000 hapa kudhibiti kwake ni kutoa elimū ya viashiria vya ugonjwa wa Ebola kuanzia kwa waganga wafawidhi, watendaji wa kata, vijiji na waendesha bodaboda,” amesema.
Kauli ya Ummy imekuja tayari serikali ikiwa imetoa msimamo wake kuwa haitafunga mipaka.
Pia Waziri Ummy amesema jicho la serikali kwa sasa lipo Mkoa wa Kagera kuhakikisha ugonjwa wa Ebola unadhibitiwa kuingia nchini kwa kuuwezesha mkoa huo, rasilimali fedha, wataalamu wa kutosha kukabiliana na ugonjwa huo wa mlipuko, vifaa tiba pamoja na gari tatu maalum za kubeba wagonjwa ‘Ambulance’.