Miradi 108 ya jamii mambo safi Mwanza

Takribani miradi 108 ya jamii wilayani Misungwi mkoani Mwanza, yenye thamani zaidi ya Sh billioni 1.9 iko ukingoni kukamilika, huku wananchi wakiipongeza serikali kwa hatua hiyo.

Ni miradi inayotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii nchini (TASAF), kama sehemu ya mpango wa kunusuru kaya maskini, awamu ya tatu ya kipindi cha pili, iliyoanza mwaka 2020 na itamalizika 2025.

Mratibu wa TASAF Halmashauri ya Misungwi, Gloria Buname, amesema miradi nane ni ya mabwawa kwa ajili ya mifugo kunywa maji, maarufu kama ‘lambo’ na 100 ni ya barabara.

“Wananchi ndio wanaoibua miradi hiyo kulingana na vipaumbele vyao katika maeneo wanayoishi, lakini inatekelezwa na wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya maskini.

“Mfuko unawalipa ujira wa shilingi 3,000 kwa siku. Wanafanya kazi kwa saa nne kwa siku, ndani ya siku 10 tu kwa mwezi, lakini wakishatekeleza miradi inakua ya kila mwanajamii,” amesema.

Wananchi kijiji cha Mwakalima, Kata ya Kanyelele, ni miongoni mwa wanufaika wa lambo, ambao wamesema licha ya mifugo kupata huduma ya maji wakati wote, wanaendesha kilimo cha umwagiliaji pia.

“Kwa hiyo tunalima hata wakati wa kiangazi. Lakini pia lambo linatupatia maji ya kufyatulia tofali za kuboresha makazi yetu,”amesema mmoja wa wananchi hao, Theresia Mayaka.

 

Habari Zifananazo

Back to top button