Miradi 630 ya uwekezaji yasajiliwa TIC

Miradi 630 ya uwekezaji yasajiliwa TIC

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema katika mwaka wa fedha 2021/2022 miradi mipya ya uwekezaji 630 yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 3.68 inayotekelezwa na makampuni ya India ilisajiliwa kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).

Amesema hatua hiyo inatokana na jitihada mbalimbali za kuboresha mazingira ya uwekezaji zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk Samia Suluhu Hassan, hivyo, ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji wengine kutoka nchini India waje wawekeze Tanzania.

Majaliwa ameyasema hayo leo Alhamisi Januari 19, 2023, wakati alipokutana na ujumbe wa Bunge la India (Lock Sabha) ulioongozwa na Spika wa Bunge hilo,  OM Birla.

Advertisement

Waziri Mkuu alikutana na viongozi hao  kwa niaba ya Rais Samia ambaye yupo nje ya nchi kikazi.

Amesema India na Tanzania zimekuwa na ushirikiano Mkubwa wa kiuchumi na biashara, huku India ikishika nafasi ya tatu kwa kuwa na ushirikiano wa biashara unaofikia Dola za Marekani bilioni 4.58 kwa mwaka 2021-2022.

Waziri Mkuu amemuhakikishia Spika huyo kuwa Tanzania itaendeleza ushirikiano wa muda mrefu uliopo kati yake na India.

“Rais ana matumaini makubwa na ushirikiano uliopo baina ya nchi ya Tanzania na India na kwamba ushirikiano huo umekuwa na manufaa makubwa kati ya nchi zetu.”

Amesema Tanzania na India zimekuwa na ushirikiano wa muda mrefu katika sekta mbalimbali zikiwemo za uchumi, nishati, maji, elimu, afya, biashara na teknolojia na hivyo kuleta manufaa makubwa.

“Mheshimiwa Rais amefurahia ujio wako nchini Tanzania, ni matarajio yake kuwa ujio huu utakuwa na manafua makubwa baina ya nchi zetu,” amesema.

“Mwezi Juni 2022 tumeshuhudia makampuni sita kutoka nchini India yakitia saini mikataba ya miradi ya maji kwa miji 28 yenye thamani ya zaidi ya dola za Marekani milioni 500 ambayo ikikamilika itawawezesha Watanzania zaidi ya milioni sita kupata maji ya uhakika.

“Nitoe wito kwa nchi ya India ambayo kwa sasa ni Mwenyekiti wa Nchi za G 20, kuwa mtetezi wa nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania katika suala zima la mabadiliko ya hali ya hewa, usalama wa chakula, uwezeshaji wa wanawake na vijana pamoja na kupambana na athari za uviko 19”

Amesema ujio wa Spika huyo na ujumbe alioongozana nao utaboresha uhusiano baina ya Bunge la Tanzania na Bunge la India kwa wabunge na viongozi wa mabunge hayo kubadilishana uzoefu.

“Nitoe wito kwa mabunge yetu haya kuweka utaratibu wa kutembeleana na kubadirishana uzoefu, ili kukuza ushirikiano.”

Pia Waziri Mkuu ameishukuru Serikali ya India kwa ushirikiano na namna ambavyo imeendela kutoa fursa za masomo kwa wataalam wa Tanzania katika sekta mbalimbali nakuiomba nchi hiyo iendelee kutoa ufadhili huo wa masomo katika nyanja nyingine za teknolojia ya mawasiliano, afya, uhandisi, kilimo, maji, madini na gesi.