KATIKA kipindi cha miaka miwili, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) chini ya uongozi wa Dk Hussein Mwinyi, imefanikiwa kusajili miradi ya uwekezaji 181 yenye thamani ya mtaji wa jumla ya Dola za Marekani bilioni 3.056 sawa na Sh trilioni 7.127.
Hayo yalibainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), Shariff Ali Shariff, wakati wa mkutano uliofanyika kwa njia ya mtandao wa Zoom uliojadili tathmini ya miaka miwili ya Dk Mwinyi tangu aliposhika madaraka ya urais mwaka 2020/21.
Shariff amesema utekelezaji wa miradi hiyo 181 itaisaidia serikali ya Dk Mwinyi kufikia lengo la kuzalisha ajira 300,000 ifikapo mwaka 2025 kama inavyoelekezwa na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020. Katika kipindi hicho cha miaka miwili ya Dk Mwinyi, pia walifanikiwa kukodisha visiwa vidogovidogo 16 ambavyo vitaleta miradi ya uwekezaji yenye thamani ya mtaji wa Dola za Marekani milioni 377 sawa na Sh bilioni 879.4 ili kusaidia utalii kukua.
Pia alisema wameanzisha ushirikiano na baadhi ya taasisi za uwekezaji za nje ya nchi ikiwemo Rwanda, Mauritius, Misri, Mamlaka ya Uwekezaji ya Omani na wako mbioni kuingia makubaliano na Shelisheli na Singapore. Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar, Simai Mohammed Said, alisema Dk Mwinyi ni kiongozi msikivu, anapokea ushauri na amekuwa mpiga debe mkubwa ili kuhakikisha sekta ya utalii inafanya vizuri.
Alisema Dk Mwinyi mara zote amekuwa akiwahimiza kuimarisha sekta ya utalii kwa kuhakikisha wanaboresha vivutio vya utalii vilivyomo visiwani humo pamoja na kuvitangaza ili kuvutia watalii wengi. Kwa mujibu wa Simai, idadi ya watalii waliofika Zanzibar mwaka 2017 ilikuwa 433,000, mwaka 2018 walikuwa 520,000, mwaka 2019, watalii 538,000 lakini mwaka 2020 idadi ilishuka hadi kufikia watalii 260,000 kutokana na ugonjwa wa Covid-19.
“Kutokana na juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan na Dk Mwinyi hasa kupitia filamu ya Royal Tour, idadi ya watalii imeanza kuongezeka ambapo mwaka jana tulipata watalii 394,000 na wameendelea kuongezeka,” alisema Simai. Balozi wa heshima wa Brazil, Abdulsamad Abdulrahim, alisema kasi ya ukuaji uchumi Zanzibar katika kipindi cha miaka miwili imeimarika kwa kiasi kikubwa.
Abdulrahim alisema mpaka sasa ukuaji wa uchumi visiwani humo imefikia asilimia 5.1 ikilinganishwa na asilimia 1.3 mwaka 2020. Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk Abdulla Juma Saadalla (Mabodi), pamoja na mambo mengine, alisema CCM kimeridhishwa na namna serikali ya Dk Mwinyi inavyotekeleza Ilani ya CCM na ahadi alizotoa wakati wa kampeni.
Wengine waliozungumza kwenye mjadala huo ni mwanasiasa mkongwe, Hamad Rashid, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia Makini, Ameir Hassan Ameir na Mwenyekiti wa waandishi wa habari Zanzibar, Farouq Karim, ambao pamoja na mambo mengine, walisema Dk Mwinyi amefanikiwa kuendesha nchi kwa misingi ya demokrasia, ameimarisha umoja wa kitaifa na mshikamano miongoni mwa Wazanzibari.