‘Wananchi wasisimamishwe muda mrefu misafara ya viongozi’

MAKAMU wa Rais  Dk Philip Mpango, ameliagiza Jeshi la polisi nchini kutosimamisha usafiri wa umma kwa muda mrefu, wakati wa ziara ya viongozi wa kitaifa.

Ni baada ya kupata taarifa kwamba hali hiyo ilijitokeza siku ya kwanza ya ziara yake katika Wilaya za Kwimba na Misungwi, mkoani hapa, ambapo shughuli za usafirishaji zilisimama kwa saa nne.

Safari za ndani na nje ya mkoa zote zilisimama, huku waathirika wakubwa wakionekana kuwa ni wasafiri kutoka mikoa mingine kuingia Mwanza.

Vilevile baadhi ya wananchi walionekana kushindwa kuvumilia hali hiyo, wakaamua kutembea kutoka katikati ya jiji kuelekea sehemu mbalimbali za mkoa, ikiwemo Nyegezi.

Hata baada ya Makamu wa Rais kumaliza ziara yake katika siku hiyo ya kwanza jana, takribani barabara zote za katikati ya jiji la Mwanza ziliendelea kuwa na msongamano wa magari hadi nyakati za usiku.

“Hata IGP nimeshamwambia jambo hili na wakuu wa polisi mikoa yote nawaambia. Haiwezekani wananchi wasimamishwe muda mrefu eti kwa sababu mimi mtoto wa maskini Philip Mpango napita. Kwani dakika kumi hazitoshi kusimamisha magari hayo?” Amehoji Dk Mpango.

Habari Zifananazo

Back to top button