Misamaha yaichanganya Hospitali ya Mloganzila

ONGEZEKO la misamaha katika Hospitali ya Mloganzila mkoani Dar es Salaam limetajwa kusababisha mapato kupotea na hivyo hospitali kutofanya vizuri katika utendaji wake.

Ukaguzi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) umebainisha hayo katika ripoti yake ya ukaguzi wa mwaka 2021/2022 ambapo pamoja na maeneo mengine, alikagua ufanisi wa taasisi za umma katika sekta ya afya.

Ripoti hiyo imesema wakati wa tathmini yake ya utendaji kazi wa Hospitali ya Mloganzila, alibaini gharama zilizidi mapato kwa asilimia saba hadi 19 kutoka 2018/19-2021/22.

Aidha, nakisi kwa mwaka iliongezeka kutoka Sh bilioni 1.92 mwaka 2018/19 hadi Sh bilioni 5.81 mwaka 2021/22 sawa na ongezeko la asilimia 394.

“Sababu za hospitali kutofanya vizuri ni mapato yanayopotea kutokana na kuongezeka kwa misamaha ambayo wakati mwingine haidhibitiwi vizuri,” alisema CAG.

Sababu nyingine ni kuongezeka kwa madai yanayokataliwa na Mfuko wa Bima ya Afya kutoka kwenye huduma zilizotolewa na hospitali hiyo na huduma duni kwa ajili ya kulaza wagonjwa binafsi na wale wa umma.

Imeelezwa kuwa utendaji duni unaweza kusababisha kuzorota kwa huduma za afya hospitalini kutokana na mapato duni ambayo hayawezi kukidhi gharama za uendeshaji na ugumu wa kufikia malengo ya kimkakati kutokana na kupungua kwa mapato kulingana na gharama zinazotumika.

CAG amependekeza Hospitali ya Mloganzila kuhakikisha huduma za kibingwa zinaimarishwa hospitalini hapo ili kuongeza wagonjwa binafsi na wa umma.

Vilevile ihakikishe inaendana na mwongozo wa Mfuko wa Bima ya Afya ili kupunguza idadi ya madai yanayokataliwa.

Aliitaka pia hospitali kuweka misamaha kielektroniki ili kuimarisha udhibiti wa misamaha inayotolewa.

Habari Zifananazo

Back to top button