Mishkaki yapigwa marufuku

NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Jumanne Sagini amepiga marufuku waendesha pikipiki maarufu ‘bodaboda’ kuacha kubeba abiria zaidi ya mmoja (maarufu mishikaki) kwenye pikipiki zao kwa kuwa ni hatari kwa usalama wao.

Pia, amelieleza Bunge kuwa kamwe hawezi kutoa tamko la kuruhusu bodaboda hizo kubeba abiria zaidi mmoja hata kama ni dharura ya kubeba mgonjwa kwa kuwa kufanya hivyo, pamoja na kuwa ni hatari kwa usalama wao pia ni kinyume cha sheria.

Sagini ameyasema  hayo akijibu swali la mbunge wa Sumve Kasalali Mageni aliyeitaka serikali kutoa tamko la kuruhusu bodaboda kubeba abiria zaidi ya mmoja vijijini kwa kuwa zinatumika kubebea wagonjwa.

“Naomba hili lichukuliwe kama dharura kule viijiini usafiri mkubwa wa wananchi kubebea wagonjwa ni bodaboda, na mgonjwa hawezi kubebwa mwenyewe lazima kuwe na mtu wa kumshikilia lakini sheria hairuhusu hili, naomba angalau basi iruhusiwe vijijini,” amesema.

Akijibu swali hilo, Sagini amesema sheria ya usalama barabarani inaeleza bayana ni kosa pikipiki kubeba abiria zaidi ya mmoja kwa kuwa ni hatari kwa usalama wa abiria hao.

“Mimi ni Naibu Waziri ninayesimamia masuala ya usalama wa raia siwezi kutoa tamko kuruhu hili.

Pikipiki ikibeba abiria wengi ni hatari kwao kutokana na kasi yake. Ningeshauri watumie baiskeli kubebea mgonjwa kwa kuwa inatembea taratibu,” amesema.

Habari Zifananazo

Back to top button