Misitu, madini wapewa changamoto ya teknolojia

Misitu, madini wapewa changamoto ya teknolojia

OFISI ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, imeziomba taasisi zinazosimamia rasilimali misitu na madini, kuungana kuwezesha upatikanaji wa Teknolojia ya Kijiofizikia ya Utambuzi Madini (IP), ili kudhibiti uchimbaji holela na upotevu wa misitu.

Hayo yameelezwa na Katibu Tawala wa Mkoa (RAS), Prof Godius Kahyarara, wakati akizindua kampeni shirikishi ya upandaji miti viwanja vya maonyesho ya teknlojia ya madini mjini Geita mwishoni mwa wiki.

Amesema Taasisi ya Jiolojia na Utafiti (GST), Shirika la Madini la Taifa (Stamico) na Wakala wa Misitu Nchini (TFS), wanaweza kusaidia upatikanaji wa kifaa cha IP kinachogharimu takribani Sh milioni 600 na kuondoa uchimbaji wa kubahatisha.

Advertisement

“Sisi nadhani kwetu tunavihitaji sana (vifaa vya IP),  labda wenzetu wa misitu mlifikirie hili, kuliko kupambana na kupanda miti, tupambane na kupunguza ukataji miti, tunafanyaje, tunaweza katika hizi teknolojia,” amesema na kuongeza kuwa:

“Mkoa wa Geita kazi kubwa ni kilimo na uchimbaji, na kwa bahati mbaya hivyo ndio vyanzo vikubwa vinavyoondoa misitu duniani, kilimo na madini, migodi mingi ipo porini, kwa maana ipo kwenye misitu na kilimo ni hivyo hivyo.

“Kwa hiyo utaalamu ni muhimu sana, kusaidiana ni muhimu sana, ni lazima tuheshimu sayansi, tuheshimu teknolojia, tutathimini ni vifaa gani tunatumia katika kuchimba, ni teknolojia gani tunatumia katika kilimo.”

Kamishina Msaidizi wa TFS, Dk Masota Abel, amesema nchi inapoteza hekta 372,000 za misitu kwa mwaka, hivyo wameimarisha usimamizi wa sheria na kasi ya upandaji miti na sasa wanasimamia mashamba 24 ya miti yenye hekta 510,000.

Meneja Masoko na Mawasiliano Stamico, Geofrey Meena, amesema wanaunga mkono utunzaji wa mazingira kwa kampeni ya upandaji miti kila mkoa na wamebuni mkaa mbadala wa kupikia kupunguza tatizo la ukataji miti.

/* */