SERIKALI imekamilisha rasimu ya mapitio ya mitaala mipya ya elimu ya msingi, sekondari na vyuo vya ualimu, ambayo inaonesha kuwa elimu ya lazima itajumuisha elimu ya msingi na elimu ya sekondari ngazi ya chini na itatolewa kwa miaka 10, na elimu ya msingi itakuwa elimu ya jumla kama itakavyofafanuliwa kupitia mitaala husika.
Pia rasimu ya mapitio ya Sera ya Elimu ya Mwaka 2014 Toleo la Mwaka 2023 imekamilika.
Aidha, masomo ya Kifaransa, Kichina, Kiarabu, Historia ya Tanzania na Maadili na Chakula na Lishe ni miongoni mwa masomo yanayopendekezwa katika madarasa ya elimu ya msingi na sekondari.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema serikali imeamua kutoa rasimu hizo hadharani ili kupata maoni ya mwisho ya wadau, na mwisho wa kuyapokea ni Mei 31, mwaka huu.
Profesa Mkenda aliwaeleza waandishi wa habari jana Dodoma kuwa serikali imechambua kitaalamu maoni yaliyotolewa awali sanjari na kujifunza kutoka kwenye nchi mbalimbali ili kutengeneza rasimu hizo.
Alisema leo kutakuwa na semina kwa wabunge wote kuhusu rasimu hizo na kuanzia keshokutwa hadi Mei 14, mwaka huu litafanyika Kongamano la Kitaifa jijini hapa Dodoma kuzijadili.
“Watanzania wote popote walipo wanakaribishwa kupitia rasimu hizi na kutoa maoni yao,” alisema Profesa Mkenda na kufafanua kuwa hati hizo zinapatikana katika tovuti ya wizara hiyo, tovuti ya Idara ya Habari (MAELEZO) na tovuti ya Taasisi ya Elimu Tanzania (TEI).
Katika rasimu ya Sera ya Elimu, mfumo wa elimu utajikita katika kujenga umahiri, akisisitiza utakuwa katika kupata ujuzi, maarifa, weledi, mwelekeo, mitazamo chanya, maadili na tabia kulingana na mahitaji ya taifa na ulimwengu wa kazi.
Rasimu ya sera inaonesha kuwa muundo katika mfumo rasmi wa elimu na mafunzo utakuwa 1+6+4+2/3+3+, kwa maana ya mwaka mmoja wa elimu ya awali, miaka sita ya elimu ya msingi, miaka minne ya elimu ya sekondari ngazi ya chini, miaka miwili ya elimu ya sekondari ngazi ya juu au miaka mitatu ya amali sanifu na miaka isiyopungua mitatu ya elimu ya juu.
Inaeleza kuwa umri wa kuanza darasa la kwanza umepunguzwa kutoka miaka saba hadi sita, kama ilivyo katika nchi nyingi duniani.
Pia elimu ya lazima itajumuisha elimu ya msingi na elimu ya sekondari ngazi ya chini na itatolewa kwa miaka 10 na elimu ya msingi itakuwa elimu ya jumla kama itakavyofafanuliwa kupitia mitaala husika.
Rasimu hiyo pia inaonesha kuwa elimu ya sekondari ngazi ya chini itagawanyika katika mikondo miwili ambayo ni mkondo wa elimu ya jumla na mkondo wa elimu ya amali.
Aidha, elimu ya amali itakuwa sehemu muhimu ya mfumo wa elimu na itatolewa kulingana na mitaala ya ngazi husika.
Elimu ya sekondari ngazi ya juu au elimu ya amali sanifu itakuwa hitaji la msingi kwa ajili ya kujiunga na elimu ya juu. Pia elimu ya juu itakuwa elimu baada ya elimu ya sekondari na itagawanyika katika mkondo wa elimu ya jumla na elimu ya amali.
Katika maboresho hayo, elimu nje ya mfumo rasmi itatambuliwa na watakaopitia mfumo huo watakuwa na fursa ya kujiunga na mfumo rasmi wa elimu kulingana na vigezo vitakavyowekwa.
Rasimu inapendekeza kila mtoto mwenye umri wa miaka sita na ambaye amepata au hakupata elimu ya awali, kwa mujibu wa sheria, apatiwe elimu ya lazima itakayotolewa kwa muda wa miaka 10.
Serikali itahakikisha kuwa elimu ya msingi na sekondari katika mfumo wa umma inatolewa bila ada.
Mitaala
Mapendekezo ya mitaala kwa darasa la kwanza na la pili, masomo ni Kusoma, Kuandika, Kuonesha umahiri msingi katika Lugha ya Kiingereza, Hisabati, Kuthamini Utamaduni, Sanaa na Michezo na Kutunza Afya na Mazingira.
Masomo kwa darasa la tatu hadi la sita ni Kiswahili, English, Kifaransa, Kichina, Kiarabu, Hisabati, Historia ya Tanzania na Maadili, Elimu ya Dini, Sanaa na Michezo, Sayansi na Jiografia na Mazingira.
Kwa elimu ya sekondari hatua ya chini, masomo ni Historia ya Tanzania na Maadili, Historia, Jiografia, English, Literature in English, Kiswahili, Kiarabu, Kichina, Kifaransa, Michezo, Biolojia, Kemia, Fizikia, Kilimo, Hisabati, Sayansi ya Kompyuta na Utunzaji wa Taarifa za Fedha.
Pia masomo ya Elimu ya Biashara, Ushoni, Sanaa Sanifu, Muziki, Sanaa za Maonesho, Maarifa ya Nyumbani, Chakula na Lishe, Elimu ya Dini ya Kikristo, Elimu ya Dini ya Kiislamu, Fasihi ya Kiswahili.
Elimu ya sekondari hatua ya juu ni Historia, Jiografia, Elimu ya Dini ya Kikristo (Divinity), Elimu ya Dini ya Kiislamu, Kiswahili, English, Kiarabu, Kifaransa, Kichina, Fizikia, Kemia, Bailojia, Chakula na Kishe, Sayansi ya Kompyuta, Hisabati, Hisabati Tumizi (Basic Applied Mathematics).
Mengine ni Kilimo, Historia ya Tanzania na Maadili, Michezo, Sanaa Sanifu, Muziki, Sanaa za maonesho, Ushoni, Mawasiliano ya Kitaaluma, Elimu ya Biashara, Uhasibu, Uchumi, Fasihi ya Kiswahili, na Fasihi katika Kingereza.
Wanafunzi wa kidato cha kwanza watakaoingia katika mkondo wa Elimu ya Amali na wa Elimu ya Jumla, watasoma kwa pamoja masomo matatu ya Elimu ya Michezo pamoja na masomo ya jumla yaliyopendekezwa.
Kidato cha pili, wanafunzi katika mkondo wa Elimu ya Amali watachagua michezo miwili na fani ambazo watazisoma na kubobea hadi kidato cha nne.
Lugha ya kufundishia
Rasimu ya seria inaonesha kuwa Lugha ya Taifa ya Kiswahili itatumika kufundishia katika elimu ya awali na elimu ya msingi, isipokuwa masomo ya lugha za kigeni na katika shule zitakazoomba kutumia Lugha ya Kiingereza kufundishia.
Lugha ya Kiingereza itatumika kufundishia kuanzia ngazi ya sekondari ya chini, isipokuwa somo la Kiswahili, masomo ya lugha za kigeni na katika shule za sekondari na vyuo vitakavyoruhusiwa kutumia Lugha ya Kiswahili kufundishia.
Aidha, Lugha ya Taifa ya Kiswahili itatumika kufundishia Somo la Historia ya Tanzania na Maadili ili kujenga na kuendeleza mila, desturi na utamaduni wa Mtanzania katika ngazi zote za elimu na mafunzo.