JESHI la Magereza imeanza kazi ya uboreshaji wa mitaala ya urekebu kwa wafungwa ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na mapendekezo ya tume aliyoundwa kwa ajili ya maboresho ya vyombo vya utoaji haki jinai nchini.
Hatua hiyo imefikiwa ili kuboresha baadhi ya maeneo yaliyoonekana kuwa na mapungufu ambayo yanachangia kwa namna moja ama nyingine waharifu kurudia makosa yao wanapokuwa uraiani.
Kamishna Jenerali wa Jeshi hilo Ramadhani Nyamka alisema hayo mjini Morogoro wakati alipozindua kazi ya uandaaji mitaala ya Urekebishaji tabia kwa wafungwa kuanzia ngazi ya astashahada na shahada.
Mitaala hiyo mipya itatumika kufundishia Maofisa wa Magereza na Askari kwenye Vyuo vyake ili na wao waweze kwenda kutoa mafunzo yanayostahiki ya urekebu kwa wafungwa magerezani .
“ Mheshimiwa Rais alilitaka jeshi letu la Magereza kuhakikisha taratibu au program za urekebu kwa waharifu zinafanyika kwa kiwango stahiki na kinachokubalika” alisema Kamishna Jenerali Nyamka.
Nyamka, alisema hata mapendekezo ya Tume ya Rais aliyoiunda kwa ajili ya maboresho ya vyombo vya haki jinai , moja ya mapendekezo yake yaliitaka Jeshi la Magereza liboreshe mitaala yake na lengo nikuwa kuwa na program za urekebishaji.
Alisema , mitaala hiyo inayohuiswa itaweza kuwarekebisha wafungwa wanaoingia gerezani, wamalizapo vifungo vyao na kurudi uraiani kuijunga na watanzania wengine katika shunguli za ujenzi wa uchumi wa Taifa ili waonekane wamerekebika.
Kamishna Jenerali wa Jeshi hilo , alisema kazi ya urekebishaji waharifu ni kazi ya kitaalam, hivyo inahitaji miongozo na mitaala inayoakisi hali ya sasa na inayoendana na wakati.
Alisema , mapitio ya mitaala , mafunzo sahihi kwa maofisa wa magereza na askari katika tasnia ya urekebu yanatakiwa kupewa uzito unaostahili ndani ya jeshi hilo.
“ Moja ya kielelezo cha kuonesha wamerekebika ni kuodokana na tabia ya urudiaji wa kutenda makosa ambayo yanawarudisha tena gerezani. “ alisema Nyamka.
“ Kwa sasa tumeona turekebishe mitaala kwa kushirikiana na Nactvet ,Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima Mamakala ya Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta) na timu ya wataalamu wa magereza kwa kukaa pamoja ili waje na mitaala ambayo imejitoshereza.” alisema Nyamka.
Kamishna Jenerali Nyamka ,alisema licha ya maboresho ya mitaala, jamii ina jukumu kubwa la kuwasaidia wafungwa wanaomaliza vifungo vyao ambao tayari wanakuwa ujuzi ili waweze kujitegemea kiuchumi na sio kuwanyanyapaa.
“ Wakati mwingine mfungwa anapotoka gerezani kwa kutumia programu za urekebu gerezani, amekuwa na taaluma ama ujuzi ambao alipoingia hakuwa nao, anapotoka ni fundi seremala mzuri, jamii iwe na utayari kuwasaidia” alisema
Nyamka ,alishauri jamii iwasaidie watu hao wenye ujuzi vitendea kazi ambapo nni njia bora ya kumtengenezea mazingira ya kuendeleza ujuzi wake na kuweza kudumu maisha ya kila siku na kufanya tatizo la urudiaji wa makosa ufumbuzi wa kudumu .
“ Jamii kwa upande mmoja iwe tayari kuwasaidi na kwa upande wapili Jeshi la Magereza lenyewe litaendelea kuboresha mitaala na kwamba tatizo hilo litakuwa limekwisha kabisa” alisema Nyamka.
Naye Kaimu Meneja wa Ukuzaji Mitaala, Utafiti na Upembuzi Yakinifu kwa Soko wa Baraza la Taifa na Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET), Dk Magreth Shawa alilipongeza Jeshi hilo kwa kufuata taratibu na miongozo ambayo imewekwa na Baraza .
Miongozo hiyo ni pamoja na kuhuisha mitaala ili iendane na kuzalisha watu wanaoweza kuajirika kwenye Magereza na kufanya kazi ambazo ni za kurekebisha wafungwa ili wanaomaliza vifungo vyao waweze kujitegemea na kutokurudia makosa.
“ Mitaala inakuwa na sehemu tatu, inarekebisha akili ya mtu, inarekebisha mikono ya mtu jinsi ya kutenda na inarekebisha mtizamo lazima abadilike” alisema Dk Shawa.
Dk Shawa, alisema kama ilivyo sasa wengi wa wafungwa wakitoka gerezani na kwenda kwenye jamii ,watu wanawaogopa wanawanyanyapaa ,lakini tunataka wakitoka huo mtaala uwe umewasaidia kiujuzi ili wasirudie tena makosa wakiwa uraiani.