MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imeandaa vitini kwa ajili ya maandalizi ya mitaala mipya inayoanza Januari mwakani kabla ya kuandaa vitabu ili wanafunzi wapate mafunzo.
Meneja Uhusiano wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta), Sitta Peter amesema hayo alipozungumza na HabariLeo.
Amesema wameanza kuandaa vitini kutokana na uharaka wa mafunzo hayo yanayoanza Januari kwenye shule za sekondari.
Amesema kwa sasa wameshakamilisha mitaala hivyo wataendelea kuandaa vitabu.
“Kwa hiyo tunatumia fursa hii kuwaelimisha wananchi au kuwafahamisha wajiandae na waandae vijana wao kutumia hiyo fursa kwa maana kwamba,
“Kuwapa ushauri wa namna wa kufanya maamuzi kwamba anakwenda kwenye mkondo wa jumla au anakwenda kwenye mkondo wa amali na wajue kwamba kuanzia mwakani utekelezaji huo unaanza,” amesema.
Anasema kwa kufanya hivyo wanafunzi wanapokwenda kidato cha kwanza waende wakiwa wamefanya uamuzi kuwa anakwenda upande gani.
Ameeleza kuwa wananchi wanatambua kuwa serikali imefanya mabadiliko ya sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014, imefanyia marejeo lakini imekwenda sambamba na kubadilisha mitaala ya ngazi mbalimbali kuanzia shule ya awali, msingi mpaka sekondari
“Kwa upande wa sekondari mabadiliko yaliyofanyika ni kuingiza masomo ya ufundi kwamba kijana anayeingia kidato cha kwanza atakuwa na fursa ya kuchagua ama aingie mkondo wa kawaida ama amali,” amesema.