SERIKALI imeleta mitambo miwili ya kuhudumia meli na shehena katika Bandari ya Mtwara kwa lengo la kuongeza ufanisi wa utendaji kazi katika bandari hiyo.
Vifaa hivyo vimewasili leo bandarini Mtwara vikiwa vinatokea Bandari ya Dar es Salaam na Tanga.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurungezi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Nchini (TPA) mara baada ya meli iliyobeba vifaa hivyo kuwasili, Meneja Uhusiano wa Mamlaka hiyo Nicodemus Mushi amesema vifaa hivyo ambavyo ni mitambo ya kupakua na kupakia mizigo bandarini imeletwa kufuatia maagizo ya Raisi Samia Suluhu Hassan aliyotoa kwa Mamlaka ya Bandari kuongeza vifaa katika bandarini Mtwara kuongeza ufanisi.
“Viifaa hivyo vimeletwa Mtwara kufuatia maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa kwa Mamlaka ya Bandari nchini mwezi Septemba mwaka jana alipotembelea bandari hii kukagua matokeo ya uwekezaji ambao serikali imefanya kwenye bandari hii,” amesema.
Akiongea kwa niaba ya Mkurungezi wa Huduma za Uhadisi Bandari ya Mtwara, Humphrey Kiwia amesema mitambo iliyoletwa inae uwezo wa kuhudumia tani 100.
Serikali imekuwa ikifanya maboresho zaidi ya Bandari ya Mtwara ambapo mpaka sasa zaidi ya Sh bilioni 157 imetumika kuboresha bandari hiyo ambayo Kwa sasa ina uwezo wa kuhudumia tani 100,000 ya mizigo kwa mwaka.
Kabla ya uboreshaji ikiwemo ujenzi wa gati Jipya, Bandari ya Mtwara ilikuwa na uwezo wa kuhudumia tani 400,000 tu ya mizigo kwa mwaka.