Miti 5,000 kupandwa Mto Msimbazi

JUMLA ya miti 5,000, itapandwa katika Mto Msimbazi uliopo jijini Dar es Salaam kwa muda wa siku tano ikiwa ni hatua ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa utunzaji wa mazingira.

Meneja Mawasilino wa Mfuko wa Uhifadhi wa Wanyamapori na Mazingira Duniani (WWF), Joan Itanisa amesema wametambulisha kampeni mpya ya kutoa dakika 60 kwa ajili ya uhifadhi wa mazingira ,ambapo wanahamasisha watu walau kwa mwaka mmoja watoe dakika 60 wawekeze kwenye uhifadhi wa mazingira.

Amesema ili kufanikisha kampeni hizo wamepanga Jumamosi Machi 25,2023  watakuwa eneo la Pugu Mnadani, ambako ni chanzo cha mto Msimbazi.

“Tutakuwa pale tutafanya usafi, lakini pia tutapanda miti 5,000 kwa wiki moja kuanzia Machi 25,2023 lakini pia tunahamsisha watu ambao hawawezi kufanya kitu mahali alipo afanye kitu ndani ya dakika 60 kwa ajili ya mazingira kama ni kupanda miti, kuelimisha watu, kufanya usafi na vitu vingine, ili kuhamasisha uhifadhi wa mazingira,”amesisitiza.

Amebainisha kuwa kampeni za shughuli za upandaji miti, kufanya usafi, kuhamasisha matumizi bora ya ardhi itaendelea miji yote, ambapo pia ofisi za WWF  zipo ambako ni Arusha ,Iringa, Masasi,Bunda, Kilwa na Mafia.

“Tunashirikiana na TBL katika bonde  la Mto Msimbazi tunavyopanda tunapanda na wanajamii na wanakuwa na umiliki mfano Pugu kuna vikundi vya vijana na wao watasimamia kuhakikisha miti inahifadhiwa na kukua

“Watakuwa na jukumu la kumwagilia na pia mamlaka ya misitu tunashirikiana nao na kila sehemu tunaangalia aina ya miti na asili ya eneo tunao wataalamu na pia kuna wataalamu wa TFS,” amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkaazi wa  WWF ,Dk Amani Ngusaru amesema wanataka watu wote washiriki katika uhifadhi wa mazingira  na kila Mtanzania aseme anatenga saa moja na familia yake, ili kusaidia Dunia ambayo inachechemea.

Ameeleza kuwa Mabadiliko ya tabianchi yana uwezo wa kubadilisha vitu vingi duniani, ikiwepo vipindi kama masika na kiangazi,ukame na bahari na anga ni vitu vya kuangaliwa sana.

Habari Zifananazo

Back to top button