HALMASHAURI ya Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita imefanikiwa kupanda miti 913,125 kwa mwaka wa fedha 2022/23 sawa na asilimia 60.9 ya agizo la serikali kwa kila wilaya kupanda miti milioni 1.5 kwa mwaka.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Mbogwe, Jacob Rombo ametoa taarifa hiyo wakati akisoma risala ya utii mbele ya viongozi wa mbio za mwenge kitaifa 2023 katika Kijiji cha Shinyanga A, ambapo miti hiyo imepandwa wadau.
Amebainisha, wanufaika wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ambao wamepanda miti 261,512, shule za msingi, sekondari na Ruwasa wamepanda miti 327,317 huku watu binafsi wamepanda miti 324,296.
Ofisa Mazingira Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe, Juma Maliseli akizungumza katika shamba la miti la wanufaika TASAF katika kijiji cha Nyasato, Kata ya Nyasato amesema mradi huo umetekelezwa na wanufaika 80 wa TASAF na shamba hilo lina ekari tatu.
“Kupitia mradi huu walengwa wamepata ujuzi na utaalamu wa kutekeleza miradi ya upandaji miti, ambapo mradi hadi kukamilika umegharimu shilingi milioni 9.5,” amesema.
Ofisa Mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, James Chuyi amesema kupitia mbio za mwenge wa uhuru mwaka 2023 wanapita na kukagua miradi ya upandaji miti kuhakikisha lengo la uhifadhi misitu linafikiwa.
Amesisitiza Watanzania kila mmoja kwa nafasi yake kutambua na kuunga mkono kwa vitendo kampeni ya kupanda miti kabla na baada ya kukata miti ili kufikiwa azma ya serikali kuimarisha ustawi wa misitu na mazingira.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa 2023, Abdalla Shaibu Kaimu ameelekeza usimamizi thabiti wa mashamba ya miti inayopandwa ili kuwezesha miti milioni 1.5 inayoelekezwa kupandwa kila wilaya ikue kikamilifu.