Miti ya asili, pombe za kienyeji kudhibiti wadudu kwenye kahawa

DAR ES SALAAM: VIUATILIFU vya asili visivyo na kemikali pamoja na mitego inayotumia vileo vya kienyeji vimeweza kudhibiti wadudu waharibifu wa kahawa aina ya mapembe, kimatira na ruhuka.

Mtafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kahawa Tanzania (TaCRI), Dk Leonard Kiwelu ameelezea hayo kama mchango wa sayansi, teknolojia na ubunifu katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii hapa nchini.

Amesema taasisi hiyo ilifanya utafiti na kugundua viuatilifu hivyo vya asili ambavyo vinatumia mimea ya utupa na mwarobaini vina uwezo wa kudhibiti wadudu hao, ikiwa ni mbadala wa matumizi ya ‘frofenoros’ ambayo imezuiliwa kutumika kwenye kahawa.

Advertisement

Ametaja aina za pombe za kienyeji zinazotumika katika mitego hiyo  kuwa ni mbege, dengulua, ulanzi na rubisi ambazo zimekuwa chambo cha kuwatega wadudu hao waharibifu wa kahawa.

Amesema tayari bustani 12 zenye miti hiyo ya viuatilifu aina ya utupa na mwarobaini zimeanzishwa katika wilaya ya Hai maeneo ya Shari na Uswaa.

Pia wilaya ya Moshi Vijijini mashamba hayo yameanzishwa katika eneo la Mrimbo, Uuwo na Mawanjeni, pamoja na wilaya za Lushoto, Mwanga, Rombo na Arumeru.

Ameeleza kuwa katika tafiti hizo imebainika kuwa ili mkulima wa kahawa apate faida anapaswa kuwa na angalau miti 450 ya kahawa, kila mmoja ukiwa na matawi ya msingi 25 hadi 45 yenye uwezo wa kuzaa.

 

2 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *