KATIKA kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, Wizara ya Afya imetekeleza majukumu yake kwa mafanikio makubwa.
Taarifa ya wizara hiyo inaonesha mafanikio ni pamoja na uwekezaji mkubwa uliofanyika katika miundombinu ya kutolea huduma za afya ambapo vituo vya kutolea huduma vimeongezeka kutoka 8,549 mwaka 2021 hadi 9,610 Machi 2024 sawa na ongezeko la vituo 1,061.
Hiyo inahusisha zahanati 7,999, vituo vya afya 1,170, hospitali za halmashauri 172, za wilaya 181, rufaa za mikoa 28, za mkoa 36, za rufaa za kanda tano, za hadhi ya kanda 12, maalumu sita na ya taifa moja.
Aidha, serikali imekamilisha awamu ya kwanza ya ujenzi wa hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini Mtwara na awamu ya pili ya ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato, kujenga na kukarabati miundombinu ya kutolea huduma za afya ngazi ya msingi ambapo hospitali mpya za halmashauri 127 zimejengwa.
Katika kuimarisha huduma za uchunguzi wa wagonjwa, serikali imenunua vifaatiba vya uchunguzi na matibabu ya wagonjwa vya thamani ya Sh bilioni 290.9 ambavyo vinapatikana kuanzia ngazi ya hospitali ya taifa hadi hospitali za rufaa za mikoa na halmashauri.
Vifaa vilivyonunuliwa ni MRI sita, CT Scan 32, Mini Angio suit, Fluoroscopy, Ultrasound 192, X-ray za kidijiti 199, Echocardiogram saba, pet scan na Cathlab tatu.
Huduma za kipimo cha CT Scan sasa zinapatikana katika hospitali 27 kati ya 28 za rufaa za mikoa nchini.
Hadi kufikia Machi 2024 wagonjwa 15,386 walipatiwa huduma za kipimo cha CT Scan.
Vitanda vyaongezeka
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu anasema idadi ya vitanda vya wagonjwa katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini imeongezeka kutoka vitanda 86,131 mwaka 2021 hadi 126,209 Machi 2024.
Vilevile anasema serikali imekamilisha ujenzi wa wodi 45 za wagonjwa mahututi (ICU) katika hospitali ngazi ya taifa, maalumu, kanda na mkoa na kuziwekea vifaa na vifaatiba.
“Pia serikali inaendelea na ujenzi wa ICU 28 katika ngazi ya halmashauri, 27 kati ya hizo zimekamilika na moja iko hatua ya ukamilishaji, hatua hii imeongeza idadi ya vitanda kwa ajili ya wagonjwa mahututi katika vituo vya umma kutoka vitanda 258 mwaka 2021 hadi kufikia vitanda 1,362 mwaka 2023.
Upatikanaji wa dawa na magari
Ummy anasema katika kipindi cha miaka mitatu, wastani wa shilingi bilioni 20 zimekuwa zikitolewa kila mwezi ambapo upatikanaji wa fedha hizo umewezesha kuimarika kwa upatikanaji wa dawa muhimu na bidhaa nyingine za afya aina 290 katika vituo vya kutolea huduma za afya vya umma kufikia asilimia 84 mwaka 2023 ikilinganishwa na asilimia 58 mwaka 2022.
Anasema hadi kufikia Desemba 2023 katika zahanati dawa na vifaa vinapatikana kwa asilimia 75, vituo vya afya asilimia 69, hospitali za wilaya asilimia 82, hospitali za rufaa za mikoa asilimia 93 na hospitali za taifa, kanda na maalumu asilimia 99.
“Serikali imenunua magari ya kubebea wagonjwa 727 ambapo hadi sasa 327 yamepokelewa na kusambazwa katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini ambulance (magari ya wagonjwa) hizi zinakwenda kusaidia kusafirisha wagonjwa wakiwemo akinamama wenye changamoto za uzazi kwa haraka na kuwafikisha katika huduma za rufaa na hivyo kupunguza adha kwa wananchi na kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika.
Idadi ya watumishi yaongezeka
Anasema wataalamu 35,450 wa kada mbalimbali wameajiriwa na kusambazwa katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini katika kipindi cha kuanzia mwaka 2021 hadi 2023.
Aidha, jumla ya ajira za mikataba kwa watumishi wa afya 2,836 kupitia miradi mbalimbali ya serikali zilitolewa.
“Jumla ya madaktari bingwa nchini hadi kufikia mwaka 2023 wamefikia 2,464 ukilinganisha na madaktari bingwa 805 mwaka 2020.
Ummy anasema serikali imeendelea kuimarisha upatikanaji wa wataalamu wabobezi kwa ajili ya utoaji wa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi kwa kuanzisha Dk Samia Super Specilized Scholarships ambapo hadi sasa, wataalamu 1,211 wamepata mafunzo hivyo kuongeza idadi ya wataalamu hao kutoka 535 mwaka 2021 hadi 1,211 hadi kufikia sasa kiasi cha Sh bilioni 22 kimetumika kugharamia mafunzo.
Mafanikio Ukimwi, malaria na TB
Kwa upande wa ugonjwa wa Ukimwi anasema serikali imeendelea kudhibiti maambukizi ambapo katika mwaka 2023 watu 8,145,576 walipima Virusi vya Ukimwi (VVU) kulinganisha na watu 6,930,758 mwaka 2022 na watu 6,493,583 mwaka 2021 (Taarifa kutoka Mfumo wa DHIS2 2023).
“Kati ya watu waliopima mwaka 2023, watu 163,131 waligundulika kuwa na maambukizi ya VVU ukilinganisha na watu 182,095 mwaka 2022 na watu 198,042 mwaka 2021 (DHIS2 2023).
Anasema waliokuwa wanatumia dawa za kufubaza virusi vya VVU walikuwa 1,663,651 Desemba 2023 kulinganisha na watu 1,612,512 Desemba 2022 na watu 1,520,589 mwaka 2021. Mwaka 2023, vifo vitokanavyo na Ukimwi vilikuwa 22,000 kulinganisha na vifo 29,000 mwaka 2022 na vifo 25,000 mwaka 2021.
“Hadi kufikia Desemba 2023, idadi ya vituo vinavyotoa huduma ya tiba na matunzo vimefikia vituo 7,396 kutoka 7,072 mwaka 2021 na kati ya hivyo CTC kamili ni 3,572 na vituo vya huduma ya mama na mtoto (RCHS) vinavyotoa huduma ya kutoa dawa ya kufubaza VVU vipo 3,824.
Kwa upande wa ugonjwa wa malaria anasema serikali imeendelea kudhibiti maambukizi ambapo katika mwaka 2023 watu milioni 19.8 walipima malaria kati yao milioni 3.46 walikutwa nayo kulinganisha na watu milioni 18.6 waliopima mwaka 2022 na milioni 3.52 wakakutwa nayo.
“Vifo vitokanavyo na malaria vilikuwa 1,540 mwaka 2023 ukilinganisha na vifo 1,735 mwaka 2022 na vifo 1,882 mwaka 2021.
Kwa upande wa ugonjwa wa kifua kikuu anasema serikali iliendelea kudhibiti maambukizi ya ugonjwa huu ambapo katika mwaka 2023 watu 440,988 walipima TB kulinganisha na watu 398,676 mwaka 2022 na watu 354,324 mwaka 2021. Waliogundulika kuwa na TB mwaka 2023 ni 90,585. Mwaka 2022 watu 100,984 walikutwa na TB na mwaka 2021 watu 60,068.
“Vifo vitokanavyo na TB vilikuwa 18,100 kulinganisha na vifo 25,800 mwaka 2022 na vifo 26,800 mwaka 2021.
Magonjwa ya mlipuko
Mwaka 2023, visa viwili vya ugonjwa wa Marburg vilipatikana, ambapo serikali ilidhibiti kabisa kusambaa kwa ugonjwa huo hatari kwa kupitia uwekezaji wa miundombinu ya maabara ya kisasa mkoani Kagera.
“Nchi yetu iliweza kupambana na janga la Marburg kwa kugundua mapema na kuudhibiti ndani ya siku 69, hii ikiwa ni historia ukilinganisha na nchi za jirani kama Uganda iliyotumia siku 113 na Equtorial Guinea siku 122,” anasema Ummy.
Bima ya Afya kwa Wote
Anasema serikali imefanikisha kutungwa kwa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote Namba 13 ya mwaka 2023 ambapo Novemba 19, 2023 iliwekwa saini na Rais Samia.
“Lengo ni kuwawezesha wananchi wote kuwa na uhakika wa kupata huduma za afya bila kikwazo cha fedha.”
Aidha, sheria hiyo imeanzisha mfuko wa kugharamia bima ya afya kwa kuwa na vyanzo mahususi vya fedha.
“Mfuko huo utawezesha wananchi wasio na uwezo kunufaika vilevile kutekelezwa kwa sheria hiyo kutawezesha vituo vya kutolea huduma za afya kuwa na mapato ya uhakika na hivyo kuboresha huduma za afya zitolewazo kwa wananchi.