Miundombinu vyuo vikuu kukarabatiwa

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA)

SERIKALI imetangaza kufanya ukarabati wa miundombinu chakavu katika vyuo vikuu vya umma kote nchini, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda amesema.

Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mwantum Mzamilu Zodo, bungeni leo, Profesa Mkenda amesema Serikali inatambua changamoto ya uchakavu wa miundombinu katika Vyuo Vikuu vya Umma nchini.

“Ili kutatua changamoto ya uchakavu wa miundombinu vyuoni, Serikali imefanya ukarabati wa miundombinu mbalimbali katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi, Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya na Chuo Kikuu cha Ardhi,” amesema.

Advertisement

Profesa Mkenda ameeleza kuwa Serikali kwa sasa inaendelea na ukarabati wa miundombinu chakavu na ujenzi wa miundombinu mipya katika Vyuo Vikuu vyote vya Umma 14 na Taasisi 5 za Elimu ya Juu zilizopo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango ili kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji vyuoni.

“Taasisi hizo zimekwisha pokea fedha kwa ajili ya kuendelea na ukarabati na ujenzi wa miundombinu kupitia Mradi wa Mageuzi ya Uchumi katika Taasisi za Elimu ya Juu (HEET),” amesema