SERIKALI imeahidi kuendelea kuboresha miundombinu ya barabara, ili kufungua shughuli za kiuchumi, ambapo kwa sasa miudombinu ya barabara za wilaya zimeimarishwa kutoka asilimia 15 mpaka asilimia 25.
Hayo yamesemwa na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Victor Seff, leo Oktoba 3,2022 jijini Dodoma, wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali na mwelekeo wa utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
“Takwimu zetu zinaonesha kuwa asilimia 75.67 ya mtandao wa barabara za wilaya ni za udongo na zinaathirika sana wakati wa misimu ya mvua na kusababisha maeneo mengi kutofikika,” amesema Mhandisi Seff.
Amesema kuwa mipango ya TARURA ni kuhakikisha inaboresha mtandao wa barabara za wilaya, angalau ziweze kupitika misimu yote.
Amesema kuwa ili kupunguza gharama katika kukamilisha mirada mbalimbali ya ujenzi, wataweka kipaumbele katika matumizi ya malighafi zinazopatikana maeneo ya kazi.